Sifa zinazozolea kanga umaarufu

Sifa zinazozolea kanga umaarufu

Na HAWA ALI

MIONGONI mwa mavazi ya Uswahilini, vazi la kanga ni maarufu zaidi. Kanga ni aina ya kitambaa cha pamba chenye umbo la mstatili na hugawanywa katika sehemu tatu.

Kwanza ni pindo yaani sehemu za ukingoni mwa kanga, pili ni mji yaani sehemu ya kati kati ya kanga na sehemu ya tatu ni ile yenye jina la kanga/msemo wa kanga aghalabu huwa sehemu ya chini ya kanga kabla ya ukingo wa chini.

Kwa kawaida kanga huwa na rangi zenye kung’aa kama vile kijani, manjano, pinki, bluu, samawati n.k na huwa katika pea/jozi.

Wavaaji hasa huangalia uzuri wa kanga kulingana na michoro na rangi ya kanga katika sehemu ya mji, na muhimu zaidi msemo wa kanga.

Kanga aghalabu ni vazi linaloenziwa na wanawake haswa wa uswahilini. Huvaliwa na rika zote kuanzia wasichana wadogo, watu wazima na hata wazee.

Mara nyingi kila mwanamke huwa na jozi kadhaa za kanga. Husemekana kwamba kanga ni vazi la mwanamke kutoka kuzaliwa mpaka kufa; Mtoto anapozaliwa hufunikwa kanga, anapofika rika la kubaleghe pia huzawadiwa na kuvishwa kanga, anapoolewa vile vile huzawidiwa kanga na hata anapokufa jeneza lake hutambulika kwa kufunikwa kanga.

Kanga ina matumizi mengi sana. Baadhi ya matumizi yake ni; Kwanza, kufungwa kiunoni hasa mtu anapokuwa nyumbani sawa na inavyotumiwa aproni jikoni katika tamaduni nyingine.

KUSWALI

Pili, kanga mbili; moja ikiwa imefungwa kiunoni na ya pili ya kujitanda juu kutoka kichwani hadi kiunoni hutumiwa kama vazi la kuswalia kwa Waislamu.

Tatu, wanawake wanapoenda kuliko na misiba hujifunga au kujitanda kanga, hii ni kama namna ya kujisitiri au vazi la heshima. Nne, kama vazi la sherehe.

Watu wanapoenda harusini aghalabu huwa na sare ya kanga hususan yenye maneno ya furaha. Tano, kama kilemba. Kanga hutumiwa kufunga kichwani kama kilemba hasa kwa wanawake. Sita, kama mbeleko. Ni kawaida kuwaona akina mama wamewafunga watoto mgongoni kwa kutumia kanga.Saba, kama taulo.

Kitambaa cha kanga ni cha pamba kama tulivyokwishasema awali. Sifa hii hufanya kanga kuwa kitu muafaka wanachotumia watu kujifutia maji wanapotoka kuoga sawa na itumikavyo taulo.

Nane, kushonea nguo. Kanga hutumiwa kushonea nguo mbalimbali kama vile gauni au sketi. Tisa, kama nepi kwa mtoto mchanga.

Kanga kuu kuu huwa na sifa ya ulaini. Aghalabu hukatwa katika vipande vidogo vidogo kiasi na kukunjwa katika umbo la pembe tatu na kutumiwa kama nepi kwa mtoto.

Mwisho, kumfunikia mtoto; kanga hutumiwa sana kumfunikia mtoto, hasa mtoto anapozaliwa. Kanga kuu kuu hutumiwa kutokana na sifa yake ya ulaini na hivyo kuwa faafu kwa ngozi changa ya mtoto.

You can share this post!

MARY WANGARI: NHIF yahitaji mageuzi ili kuboresha huduma

‘Wasanii Wazoefu’ mboni ya sanaa chuoni Gretsa, Thika