PENZI LA KIJANJA: Sigeuze bedirumu afisi yako!

PENZI LA KIJANJA: Sigeuze bedirumu afisi yako!

Na BENSON MATHEKA

JIMMY alikuwa na mazoea ya kufanyia kazi katika chumba cha kulala hadi juzi alipogundua kuwa tabia yake ilikuwa sumu kwa uhusiano wake na mkewe.

Anasema kwamba mwenzake alianza kulalamika akidai anampuuza.

“Nilikuwa nikifanyia kazi chumba cha kulala usiku mke wangu akiwa amelala kitandani. Juzi, alinikabili na kunitaka niamue mambo mawili; chumba cha kulala kiwe ofisi au cha faragha,” asema Jimmy.

Kufunguka kwa mkewe kulimfungua macho akabaini alikuwa akikosea. “Masuala ya kazi hayafai kuchukua nafasi kubwa katika uhusiano wa mapenzi. Japo kazi ni muhimu, chumba cha kulala kinafaa kuwa cha faragha kati ya mtu na mpenzi wake,” asema mshauri wa masuala ya mapenzi Tika Sandu.

“Usipeleke masuala ya kazi katika chumba cha kulala. Yabaki sebuleni au afisini. Kazi ya chumba cha kulala ni kufurahishana na ukianza kukitumia kwa shughuli za kazi, kitakosa maana yake na kuvuruga uhusiano na mpenzi wako,” aeleza Sandu.

Mtaalamu huyo anasema kwamba hii ndio sababu kuna mavazi spesheli na mepesi ya chumba cha kulala.

“Pia unatakiwa kuingia chumba cha kulala ukiwa safi. Safisha meno ili kuhimiza mtu wako kuchangamkia mabusu na kukupakata, ambazo ni shughuli muhimu za chumbani,” asema Sandu.

Kulingana na Dennis Kariuki, mshauri wa masuala ya mahusiano katika kituo cha Maisha Mema, Nairobi, kushabikia kazi wakati unapaswa kuwa unamdekeza mtu wako kunaweza kuvuruga penzi lenu.

“Tenganisha shughuli za kazi na za mapenzi. Mtu wako anataka kusikia maneno matamu ya kuchombeza mapenzi kitandani. Anataka umkaribie, umkumbatie ili ahisi joto lako muweze kuchangamkiana na kurushana roho. Ukibeba kazi hadi chumbani, unaashiria kuwa hauna muda naye na anaweza kukutema au kutafuta joto hilo pembeni,” asema.

Kariuki anasema watu wanafaa kupunguza matumizi ya simu za mkono na vifabebe katika chumba cha kulala.

“Mchumba wako anahitaji umpe muda wako. Chumba cha kulala kimetengwa kwa shughuli za faragha kati ya mtu na mpenzi wake,” asema.

Wataalamu wanapendekeza kuwa iwapo wachumba wana mtoto, wamtengee chumba tofauti na chao cha kulala iwapo wana uwezo wa kufanya hivyo.

“Mtoto akifikisha umri wa kuweza kulala peke yake, mtengee chumba chake salama na karibu na chumba chenu cha kulala. Hafai kuishi ndani ya chumba chako ambacho kinafaa kuwa kisiwa cha wawili- wewe na mchumba wako,” asema Sandu.

You can share this post!

Vicoty Chepng’eno azoa taji la Houston Half Marathon...

Refa Alex Kenyani anayepania kuwa kama Mike Dean

T L