Makala

SIHA NA LISHE: Faida ya kula mayai

July 25th, 2019 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

Mayai hushibisha

PROTINI zilizoko ndani ya mayai kando na kuujenga mwili pia hukufanya kutohisi njaa haraka.

Ina maana kuwa ukila mayai unaweza kukaa muda marefu zaidi bila kula ikilinganishwa na mikate au vyakula vingine vya ngano.

Husaidia kupunguza uzani

Kwa kula mayai, unaweza kupunguza uzani wa mwili. Inadaiwa kuwa watu wanaokula mayai wamefanikiwa kupunguza uzani wa miili yao kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na wasioyala.

Mayai ni bei rahisi

Ukilinganisha na vyakula vingine vya protini kama vile nyama, mayai ni bei rahisi zaidi. Hivyo basi, mayai yanaweza kupatikana na kuandaliwa kwa urahisi wakati wa kifungua kinywa kuliko vyakula vingine.

Mayai ni chanzo kikubwa cha protini

Kama nilivyotangulia kusema, mayai yana kiasi kikubwa cha protini kinachohitajika katika kujenga miili yetu.

Hivyo basi, ni vyema kula mayai asubuhi wakati wa kifungua kinywa ili kujipatia virutubisho hivi.

Mayai hayaongezi lehemu (Cholesterol)

Ni dhahiri kuwa mayai yana kiwango fulani cha lehemu lakini lehemu iliyoko katika mayai inapoliwa haina athari kwenye kiwango cha lehemu kwenye damu. Hivyo hakuna haja ya kuhofu juu ya magonjwa ya moyo yatokanayo na lehemu.

Husaidia ukuaji wa ubongo na uwezo wa kumbukumbu

Kirutubisho kinachojulikana kama “Choline” kinachopatikana kwenye mayai ni muhimu katika ukuaji na maendeleo ya ubongo.

Pia kinahusishwa katika kuongeza uwezo wa ubongo wa kutunza kumbukumbu.

Hulinda macho

Kemikali za leutin na zeaxanthin zinazopatikana kwenye mayai zinaaminika kulinda macho dhidi ya madhara ya mionzi mibaya.

Kumbuka afya yako ni muhimu sana. Jali afya yako kwa kuzingatia ulaji bora.

Mayai tayari kuliwa. Picha/ Margaret Maina