Makala

SIHA NA LISHE: Manufaa mbalimbali ya karoti

July 25th, 2019 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

WATU wengi wanapenda kutumia karoti kupika mboga au nyama.

Wataalamu wa masuala ya lishe na afya hushauri kwamba ili tuwe na afya bora, tunatakiwa angalau tule karoti sita kwa wiki au moja kwa siku.

Karoti inaweza kuliwa hivyo au ikatumika katika kutengeneza juisi.

Juisi ya karoti. Picha/ Margaret Maina

Miongoni mwa faida za kula karoti ni pamoja na: kuimarisha macho kuona vizuri, kurutubisha seli mwilini, kuimarisha afya ya ngozi, kuondoa sumu mwilini, kuimarissha fizi.

Karoti husaidia kuimarisha macho kuona vizuri, hasa kwa aliye na tatizo la kutoona vizuri usiku. Pia inasaidia kuondoa matatizo ya allergy kwenye macho, mfano macho kuwasha sababu ya vumbi.

Karoti inarutubisha seli mwilini na kuzifanya zisizeeke haraka. Hii inatokana na uwepo wa Vitamini A ambayo ni muhimu katika kuimarisha uwezo wa macho kuona.

Karoti. Picha/ Margaret Maina

Huifanya ngozi iwe nzuri na yenye afya. Ikiwa unataka kuitumia kurutubisha ngozi yako, ikwangue kiasi unachotaka kisha tia asali kijiko kimoja, mafuta ya nazi au ya mizeituni kijiko kimoja na limau kijiko kimoja.

Changanya vizuri, kisha itumie kusugua mwilini sehemu yoyote unayotaka. Ukishamaliza, acha kama robo saa kisha oga. Hii itaifanya ngozi iwe laini na kuondoa mikunjo katika ngozi.

Karoti husaidia kuondoa sumu na taka mwilini, inaondoa mafuta yasiyotakikana na kuliwezesha lifanye kazi vizuri, pia husafisha njia ya haja kubwa.

Karoti zinasaidia kufanya fizi na meno kuwa imara na kusaidia uzalishwaji wa mate.

Karoti hupunguza hatari ya kupata Shinikizo la Damu (blood pressure) kwani ulaji wa karoti husaidia mwili kupata madini muhimu ya Potasiamu na kufanya damu kufika katika maeneo mengine ya mwili.

Karoti pia husasidia kuzuia magonjwa mengine kama vile kisukari (Diabetes), Kiharusi (Stroke), pamoja na magonjwa ya moyo.

Vilevile karoti husaidia kuongeza kinga mwilini; immune boosters ambazo husaidia kuimarisha kinga ya mwili.

Pia karoti ina Vitamini C ambayo ni muhimu kwa kusisimua seli nyeupe za damu (white blood cells) ambazo ni sehemu muhimu katika kinga ya mwili.