Makala

SIHA NA LISHE: Sifa za mnavu

August 10th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

UTAFITI wa Kisayansi umethibitisha kuwa mmea wa mnavu husifika kwa kuwa na virutubisho spesheli vinavyokinga binadamu dhidi ya maambukizi ya maradhi kadha.

Kwa mujibu wa Afisa wa nyanjani kuhusu Kilimo katika Kaunti ya Murang’a, Bw James Thuo, mnavu ulianza kutumika na mababu zetu tangu azali.

“Ni mmea ambao umekuwa ukitumika kama mboga yenye madini muhimu kwa binadamu haswa ile ya Iron. Ni ukweli kuwa mboga ya mnavu ikichemshwa huwa na manufaa kabambe kwa wajawazito na vilevile wakishajifungua,” anasema Bw Thuo.

Anaongeza kuwa mboga ya mnavu huaminika kuwa na uwezo wa kuongeza hali ya damu kuzima kutiririka mtu apatapo jeraha.

“Ni mboga ambayo ilikuwa ikipewa mashujaa wa kivita baada ya kujeruhiwa ili kuwarejeshea nafuu ya haraka na pia nguvu ya kujikinga wasitatizwe na kizunguzungu katika harakati za kuponesha majeraha yao,” anasema.

Kwa jina lake la Kisayansi, mnavu hufahamika kama African nightshade na hufanya vyema katika kanda zote za juu na pia za chini kwa kuwa licha ya kupenda maji mengi, pia, hukubali hali ya kiangazi na huwa na mbinu yake spesheli ya kustahimili mabadiliko ya mazingira.

Jamii ya Agikuyu hutambua mmea huu kwa jina managu. Wajaluo huutambua kama osuga huku jamii ya Kipsigis ikiufahamu kama isoiyot.

Jamii ya Wakamba huutambua kama kitulu huku Wamaasai wakiupa jina la ormomoi. Nao kwa upande wa Wataita, wanaufahamu kama ndunda.

Mtafiti wa mimea katika taasisi ya teknolojia za kilimo na uimarishaji mifugo (Karlo) Bi Jayne Gathii anafafanua kuwa matawi ya mnavu ni mboga iliyo lishe bora kwa kuwa katika mazingira mwafaka zaidi, majani ya mmea mmoja uliokomaa huwa na protini, vitamini A, B, na C.

“Aidha, ni mmea ambao unatambulika kisayansi kuwa na uwezo wa kuongeza nguvu za kiume pamoja na kuwa kitulizo mwafaka kwa mgonjwa wa malaria ambaye anahisi kuishiwa na nguvu mwilini,” anasema.

Anaongeza kuwa watafiti wa dawa za kutumika kwa binadamu wamethibitisha kuwa mnavu ni mmoja wa mimea ambayo kwayo hutwaliwa chembechembe za kutengeneza dawa ya kudhibiti kuhara, magonjwa kadhaa ya macho na pia vidonda vya tumbo vinavyokita kambi katika mfumo mzima wa usagaji chakula.

 

Pichani ni mkulima Henry Kinuthia, 34, akiwa katika shamba lake la mnavu katika kijiji cha Kagongo, Kaunti ya Murang’a mwaka 2019. Picha/ Mwangi Muiruri