Makala

SIHA NA LISHE: Vyakula mwafaka kwa mama mjamzito

July 11th, 2019 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

AFYA ya mama na mtoto ni muhimu sana.

Hivo basi mwanamke anatakiwa apate chakula bora kilicho na madini yote ikiwemo vitamini na protini.

Kunde

Mbegu za kunde ni sehemu muhimu ya chakula kwa mama mjamzito kwa sababu huwa na kiwango kikubwa cha protini.

Kwa watu wasiokula nyama au wana uwezo mdogo tu kujipatia nyama, kunde zinatosheleza mahitaji ya protini.

Mayai

Mayai – angalau mawili kwa siku – husaidia kuupa mwili protini, vitamini A na madini ambayo yatasaidia kuzuia kuambukizwa na maradhi mbalimbali.

Maziwa na bidhaa zitokanazo na maziwa

Glasi moja au zaidi ya maziwa ya aina yoyote pamoja na/au vyakula jamii ya maziwa kama mtindi na siagi ni muhimu.

Maziwa ni muhimu kwa protini, calcium, vitamini na virutubisho vingi vinginevyo.

Vitasaidia ukuaji wa mifupa na misuli, Ni muhimu pia kwa damu yenye afya, husaidia katika mtu kupata usingizi na kusawazisha mdundo wa moyo au mapigo ya moyo.

Viazi tamu

Viazi vitamu vina vitamini A ambayo husaidia ukuaji wa macho ya mtoto, ngozi na mifupa

Nyama

Nyama ya kuku au ya ng’ombe huwa na protini nyingi sana na husaidia katika ukuaji wa mwili wa mtoto hasa kwa mama mjamzito wa miezi minne.

Nafaka na vyakula vya wanga

Vyakula hivi huipa mwili nguvu ya kufanya kazi na pia ukuaji wa mtoto tumboni.Vyakula hivi ni kama mahindi,mtama ,mihogo,vyakula vya ngano kama mkate na kadhalika.

Parachichi

Ni matunda ambayo yana mafuta mengi maarufu kama fatty acid. Parachichi linasaidia katika ukuaji wa ubongo, ngozi nyororo na ukuaji wa misuli ya mtoto angali katika chupa tumboni mwa mama mjamzito.

Mboga za majani

Mboga za majani kama spinachi na kabeji ni muhimu kwa mjamzito.

Mboga hizi zinafaa ziwe zile za rangi ya kijani kwa sababu hizi ndizo zenye virutubisho vya kutosha.

Mboga hizi zitampa mama na mtoto wake Vitamini A na B, pia virutubisho vitakavyosaidia mwili kupata protini ya kutosha, ukuaji wa mwili, na utengenezaji wa damu.

Kutopata mboga za kutosha kunaweza sababisha mama kupata ugonjwa wa Anemia.

Mafuta ya samaki

Mafuta ya samaki huwa na Omega fatty acids ambazo husaidia ukuaji wa ubongo na macho ya mtoto.

Maji

Maji ni muhimu kwa mwili kwa sababu inasaidia kwenye mmenyenyo wa chakula na pia husaidia kuzia choo ngumu.

Maji pia huzuia uvimbe wa mwili na maambukizi ya mfumo wa mkojo (UTI).