Makala

SIHA NA LISHE: Vyakula vinavyoimarisha uwezo wa kuona

July 26th, 2019 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

KULA vizuri kuna manufaa mengi kwa ajili ya miili yetu.

Kando na karoti, kuna virutubisho mbalimbali vinavyohitajika kwenye macho.

Samaki

Samaki ni bora kwa afya ya macho kwani ni chakula ambacho kina mafuta ya Omega-3 ambayo ni muhimu kwa ajili ya kuzuia macho angavu (kunyauka kwa macho), na hali ya kudhoofika kwa misuli ya macho. Kama umeshindwa kula vyakula hivi vya baharini unaweza kula matunda kama vile matunda damu ili kupata Omega-3.

Mboga za majani

Mboga muhimu kwa afya. Picha/ Margaret Maina

Watu wengi hufikiri kuwa kula mboga za majani ni dalili za umaskini; lakini ukweli ni kuwa mboga za majani zina manufaa makubwa kwenye miili yetu.

Mboga za majani zina kemikali ya luteini na zeaxanthini ambazo ni muhimu katika kulinda na kujenga uwezo wa macho kuona vizuri.

Mayai

Mayai yana manufaa kwa ajili ya afya ya macho na miili yetu kwani yamejaa vitamini. Vitamini A inayopatikana kwenye mayai hulinda macho dhidi ya kutokuona usiku pamoja na kukauka kwa macho (macho angavu).

Matunda jamii ya mchungwa na zabibu

Matunda kama vile malimau, machungwa na zabibu yamesheheni vitamini C. Hivyo, yatawezesha macho yako kujikinga na magonjwa kama vile kudhoofika kwa misuli ya macho.

 Karanga na jamii zake

Vyakula hivi vimejaa mafuta aina ya Omega-3 na vitamini E ambavyo kwa pamoja ni muhimu kwa ajili ya afya ya macho.

Matunda ya rangirangi

Chakula kama karoti, nyanya, pilipili mboga, na mahindi ni vyanzo bora vya vitamini A na C.

Inaaminika kuwa kemikali ya carotenoids inayoyapa matunda haya rangi zake ni muhimu kwa afya ya macho.

Vyakula vya jamii ya kunde

Vyakula vya jamii ya kunde vina kemikali kama vile Bioflavonoid na Zinc ambavo ni muhimu kwa ajili ya ulinzi wa retina na kuzuia kudhoofu kwa misuli ya jicho.

Nyama ya ng’ombe

Nyama imejaa madini ya zinc ambayo huuwezesha mwili kufyonza vitamini A ambayo ni muhimu kwa macho pia.

Ikumbukwe kuwa vitamini A huuwezesha mwili kukabiliana na matatizo yatokanayo na umri au uzee.

Nyama ya ng’ombe kabla ya kupikwa. Picha/ Margaret Maina

Kwa hakika maradhi mengi humpata mwanadamu kutokana na kuharibu au kuacha mfumo wa ulaji wa asili.

Ni kweli kuwa matunda na mboga ni ya manufaa makubwa kwa ajili ya macho yetu pamoja na mwili mzima kwa ujumla.

Jitahidi kufanya angalau nusu ya mlo wako uwe ni matunda na mboga. Usisahau pia kumwona daktari mara kwa mara ili kupima afya ya macho yako pamoja na kupata ushauri.