Makala

SIHA NA ULIMBWENDE: Jinsi ya kutumia juisi ya karoti kuondoa mikunjo kwenye ngozi

January 3rd, 2020 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

MIKUNJO katika ngozi ni miongoni mwa matatizo yanayowakabili wanawake wengi.

Tofauti na mikunjo ya uzee, mikunjo hii hutokana na kuchoka kwa ngozi kunakosababishwa na mambo mbalimbali.

Katika kupambana na tatizo hilo, zifuatazo ni njia mbalimbali zinazoweza kutumika kutatua tatizo hili.

Unashauriwa kumwona mtaalamu wa afya kwa ushauri zaidi wa matumizi ya njia hizo za asili kabla ya kuanza kuzitumia.

Unaweza kutumia viungo vinavyopatikana jikoni kwako kupambana na mikunjo katika ngozi. Baadhi ya viungo hivyo ni pamoja na:

Karoti

Tumia juisi ya karoti kwa kupaka katika ngozi yako, hasa katika maeneo yaliyoathirika.

Karoti ina virutubisho muhimu kwa ngozi yako. Pia ina uwezo mkubwa wa kuondoa sumu ndani ya ngozi.

Si hivyo tu, karoti inaweza kuondoa kabisa tatizo la mikunjo ya ngozi hasa sehemu za pembeni ya macho, shingo na maeneo kama hayo.

Namna ya kufanya

Chukua karoti, saga kwenye blenda kisha kamua ili kupata juisi yake. Tumia pamba kupaka katika maeneo yaliyoathirika, fanya hivyo mara kwa mara, itakusaidia kupunguza ama kuondoa kabisa tatizo hilo.

Maziwa

 

Maziwa yakiwa katika kibuyu na vilevile katika glasi. Picha/ Margaret Maina

Maziwa yana virutubisho vinavyochochea kunawiri kwa ngozi. Pia yana chembechembe za ‘Alfa-Hydroxide Acid’ ambazo zina uwezo mkubwa kuondoa seli zilizokufa mwilini. Hivyo vyote husaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa tatizo la mikunjo katika ngozi. Unachotakiwa kufanya ni kuchukua maziwa kiasi na kisha kuyachovya pamba ndani yake halafu taratibu unapaka maeneo yaliyoathirika.

Mshubiri; yaani Aloe vera

Jani la Aloe vera. Picha/ Margaret Maina

Jeli ya Aloe vera ndiyo hasa inayotakiwa katika shughuli hii.

Chukua jani lake na kisha likate ili kupata utomvu wake.

Chukua utomvu au jeli hiyo kama wengine wanavyoita na kisha pakaa sehemu iliyoathirika.

Itapunguza ama kuondoa kabisa tatizo hilo.