Makala

SIHA: Unywaji holela wa pombe unasababisha madhara haya…

July 16th, 2019 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

LICHA ya baadhi ya watu kuzoea pombe kama njia ya kujiburudisha, ina madhara mengi kwa afya ya mnywaji.

Watu wengi hupenda kunywa pombe vilabuni au nyumbani kwao kama njia ya kujistarehe, lakini pombe husababisha matatizo ya kiafya, yakiwemo magonjwa ya moyo, ini pamoja na majeraha yatokanayo na ajali zitokanazo na ulevi.

Licha ya kuwepo kwa kampeni kadha zinazopinga matumizi ya pombe, bado watu wengi wameendelea kushikilia kinywaji hiki bila kufahamu athari zake kwenye afya zao.

Matatizo ya moyo

Unywaji wa pombe kupindukia husababisha matatizo ya moyo ambapo mishipa ya moyo hudhoofika na kushindwa kusukuma damu.

Jambo hili husababisha damu kuganda na kusababisha kiharusi (stroke).

Tatizo la ini

Unywaji wa pombe unaweza kusababisha maradhi ya ini yajulikanayo kama Cirrhosis; ambayo ni maradhi ya ini kushindwa kufanya kazi yake kutokana na uharibifu wa muda mrefu.

Shinikizo la damu

Unywaji wa pombe kupita kiasi umethibitishwa kuchangia kwa kiasi kikubwa maradhi ya shinikizo la damu. Imebainikia kuwa pombe huathiri mfumo wa usukumaji wa damu mwilini jambo ambalo hupelekea shinikizo la damu na baadaye matatizo mengine kama figo na ini kushindwa kufanya kazi.

Ugonjwa wa anemia

Anemia ni ugonjwa unaotokana na kushindwa kwa seli nyekundu za damu kusafirisha oksijeni ya kutosha kwenda kwenye mwili.

Hivyo, unywaji wa pombe hupunguza uwezo wa seli nyekundu za damu kusafirisha oksijeni ya kutosha hivyo kupelekea ugonjwa wa anemia.

Kusinyaa kwa ubongo

Mtu anapozidi umri ndivyo ubongo wake unavyozidi kusinyaa. Hivyo, unywaji wa pombe huharakisha kusinyaa kwa ubongo na husababisha matatizo yatokanayo na kusinyaa kwa ubongo kama vile kupoteza au kupungua kwa uwezo wa kumbukumbu.

Msongo wa mawazo

Pombe huathiri mchakato wa kikemikali wa ubongo. Imebainika kuwa watu wanaokunywa pombe kupindukia hukabiliwa na msongo mkubwa wa mawazo. Msongo wa mawazo ni chanzo cha maradhi mbalimbali kama vile shinikizo la damu, matatizo ya akili, matatizo ya moyo.

Maumivu ya miguu (gout)

Gout ni ugonjwa wa miguu unaotokana na kukusanyika kwa asidi kwenye viungio vya mifupa. Mara nyingi, ugonjwa huu hujitokeza sana wakati wa baridi.

Kusinyaa kwa uso na macho

Unywaji mkubwa wa pombe husababisha kusinyaa kwa uso na macho hasa kwa wale wanaokunywa usiku. Mara ngingi uwatazamapo wanywaji wakubwa wa pombe utaona hata sura zao zimebadilika na kuonekana zimezeeka au kuchoka kuliko awali.