Sihitaji BBI kuingia Ikulu, Raila asisitiza

Sihitaji BBI kuingia Ikulu, Raila asisitiza

WYCLIFFE NYABERI na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga amejipiga kifua na kusema hahitaji msaada kupitia kwa Mpango wa Maridhiano (BBI) ili awe rais.

Akipuuzilia mbali wanasiasa wanaodai kuna njama ya viongozi wanaopigia debe marekebisho ya katiba kuitumia kama ngazi ya kuingia mamlakani kwa urahisi, Bw Odinga Ijumaa alisema akiwania urais wananchi watamchagua.

“Hii BBI sio eti ni Raila anatumia mlango wa nyuma kuingia Ikulu. Raila akitaka kuenda Ikulu wananchi watampeleka. BBI ni kitu ambacho kitadumu na kusaidia hadi vizazi vijavyo katika taifa letu,” akasema.

Alikuwa akihutubia waombolezaji waliohudhuria ibada ya mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Bonchari, Oroo Oyioka.

Ibada hiyo ilifanyika katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Itierio, Kaunti ya Kisii.

Kufikia sasa, Bw Odinga hajatangaza wazi ikiwa atawania urais mwaka wa 2022 ingawa hotuba zake za hivi karibuni zinaashiria ana mipango ya kuwania.

Gavana wa Mombasa Hassan Joho pekee ndiye amewasilisha ombi la kutaka kushiriki mchujo wa atakayepeperusha bendera ya ODM kwa urais mwaka 2022.

Chama hicho mnamo Alhamisi kiliongeza muda kwa wanaotaka kushiriki mchujo huo hadi Machi 31.

Bw Odinga akizungumza baadaye jana katika eneobunge la Ugunja, Kaunti ya Siaya, alisisitiza hatatangaza kama atawania urais hadi mpango wa kurekebisha katiba utakapokamilika.

Suala la kuwa marekebisho ya katiba ni njama ya kisiasa inayohusu urais 2022, limekuwa likivumishwa kwa muda mrefu na Naibu Rais William Ruto na wandani wake.

Mkutano ulioongozwa na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi mnamo Alhamisi ambao ulihudhuriwa na Bw Odinga, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, mwenzake wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula (Ford Kenya), uliibua upya mjadala kuhusu uwezekano wa wanaounga mkono BBI kuungana dhidi ya Dkt Ruto ifikapo 2022.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Seneta wa Baringo Gideon Moi anayeongoza Chama cha KANU, na Gavana wa Kitui Charity Ngilu aliye kiongozi wa Narc.

Katika taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo, walisema ulikuwa ni wa kujadili mipango ya kurekebisha katiba.

Ijumaa, Dkt Ruto alipokuwa katika Kaunti ya Nandi, alirejelea matukio hayo na kusisitiza hatababaishwa katika azimio lake la kumrithi Rais Kenyatta atakayestaafu urais mwaka 2022.

“Wanaume wamenipangia kule Nairobi lakini mimi niko na wananchi hapa chini. Wanatuambia watatupangia serikali kule Nairobi wakisema wale wadosi watatupangia. Mimi nawaambia serikali ya 2022 haiwezi kupangwa hivyo,” akasema.

Bw Odinga alisisitiza kuwa, mpango wake na Rais Kenyatta kuhusu BBI ni kuleta umoja wa nchi.

Alifichua kwamba Rais alikuwa amemdokezea mpango wa mabunge ya kaunti za Mlima Kenya kupitisha mswada wa urekebishaji katiba Jumanne iliyopita, na ikawa hivyo.

“Sisi tunasema Wakenya wataendelea mbele wakiwa na umoja. Gurudumu sasa limeenda kwa bunge (la kitaifa na seneti). Ikitoka kwa bunge itakuja mashinani kwa wananchi na tutakuja kuwaambia zaidi kuhusu ubora wa BBI,” akasema.

Kaunti za Nandi na Baringo pekee ndizo zimekataa kupitisha mswada huo kufikia sasa.

You can share this post!

Man-Utd wapewa AC Milan, Arsenal kuvaana na Olympiakos huku...

Trump kuhutubia mkutano akilenga kuwania tena 2024