Sihitaji kuungwa mkono na Uhuru kuingia Ikulu – Raila

Sihitaji kuungwa mkono na Uhuru kuingia Ikulu – Raila

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga kwa mara ya kwanza ametangaza waziwazi kuwa hahitaji uungwaji mkono kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta kufanikisha azma yake ya kuwa rais 2022.

Akionekana kuthibitisha kuwa atakuwa debeni mwaka ujao, Waziri huyo Mkuu wa zamani alisema hatahitaji usaidizi wa Rais Kenyatta katika jaribio lake la tano kutaka kuwa Rais wa Kenya.

“Sitaki kuidhinishwa na Uhuru au mtu yeyote. Ikiwa nitasimama nitahitaji kura hiyo moja,” Bw Odinga akasema Alhamisi asubuhi kwenye mahojiano katika Redio Citizen.

“Ikiwa nilishindana na Uhuru katika chaguzi mbili zilizopita katika miaka ya 2013 na 2017 na kila mtu anajua matokeo, mbona sasa nisubiri uungwaji mkono kutoka kwake?” akauliza.

Naibu Rais William Ruto, ambaye ametangaza kuwa atawania urais kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) baada ya kusambaratika kwa Jubilee, amedai kuwa Bw Odinga na vinara wengine wa Nasa wanamezea mate uidhinishwaji kutoka kwa Rais.

“Wale wengine tunaoshindana nao hawana mipango. Juzi nilisikia kwamba wanataka kuungwa mkono huku na kule. Ningependa kuwaambia kuwa tutawashinda kwa sababu sisi tunategemea Mungu na kura ya wananchi,” akasema.

Dkt Ruto alisema hayo mwezi jana baada ya Rais Kenyatta kuahidi kuunga mkono mmoja wa vinara wa NASA kuwa mrithi wake, endapo wataungana.

“Steve nyingi muungane katika Nasa na nitatembea na nyinyi katika uchaguzi mkuu ujao,” Rais Kenyatta akaombia kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka katika Ikulu ya Nairobi alipokutana na viongozi kutoka eneo Ukambani.

Kauli hiyo ya kiongozi wa taifa iliashiria kuwa amebadili kabisa nia yake ya hapo awali ya kumwidhinisha Dkt Ruto kama mrithi wake 2022 atakapostaafu baada ya kukamilisha muhula wake wa pili na wa mwisho, kikatiba.

Bw Odinga alipoulizwa jana kama kweli atawania urais mwaka ujao ikizingatiwa kuwa mnamo 2017 alisema alikuwa na “risasi moja pekee,” kuashiria atastaafu siasa, alikana madai hayo.

“Mimi sikusema nimebakisha risasi moja pekee. Hayo yaliyokuwa madai ya vyombo vya habari. Mimi bado niko na ‘magazine’ mzima,” akaeleza, kumaanisha kuwa bado yu tayari kuwania urais.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa ODM alifafanua kuwa atafanya uamuzi wa mwisho kuhusu iwapo atawania urais au la baada ya hatima ya mchakato wa marekebisho ya Katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI) kuamuliwa.

“Baada ya BBI ndipo nitaaamuliwa ikiwa nitawania urais au la. Hata hivyo, ni haki yangu ya kikatiba kuwania na hakuna anayeweza kunuzuia,” Bw Odinga akaeleza.

Hatima ya marekebisho ya katiba kupitia Mswada wa BBI sasa iko mikononi mwa jopo la majaji sababu wa Mahakama ya Rufaa.

Majaji hao akiongozwa na Rais wa Mahakama hiyo Daniel Musinga, watarajiwa kutoa uamuzi kuhusu kesi iliyowasilishwa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu iliyoharamisha mchakato huo. Uamuzi huo kuhusu kesi hiyo iliyowasilishwa na Bw Odinga, Rais Kenyatta na Mwanasheria Mkuu Paul Kihara, umeratibiwa kutoka Agosti 20, 2021.

Alhamisi, Bw Odinga alisema kuwa upande wake utakubali uamuzi utokaotolewa na mahakama hii “kwa sababu sisi ni wanademokrasi.”

You can share this post!

Lusaka akiri kuwa katika uhusiano wa kimapenzi na...

Wezi wa nyaya za stima bungeni taabani