Sihitaji OKA 2022 – Raila

Sihitaji OKA 2022 – Raila

Na WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga, Ijumaa alisema atawania urais mwaka 2022 Wakenya wakimwidhinisha, hata ikiwa viongozi wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA) hawatamuunga mkono.

Kwenye mahojiano na vituo kadhaa vya redio na televisheni vinavyotangaza kwa lugha ya Gikuyu, Bw Odinga alisema kuwa anachohitaji ni kukubalika na wananchi, wala si uungwaji mkono wa viongozi wala miungano ya kisiasa.

“Nitawania urais kulingana na matakwa ya Wakenya wala si viongozi wa kisiasa. Nitazingatia mwelekeo watakaonipa,” akasema Bw Odinga.

Kauli yake inajiri huku kukiwa na tashwishi ikiwa viongozi wa OKA watamuunga mkono kwenye azma yake ya urais 2022.

Viongozi hao wanajumuisha Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), maseneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) na Gideon Moi (Kanu).

Inadaiwa wanne hao wamekuwa wakishinikizwa na Rais Kenyatta kumuunga mkono Bw Odinga japo hawajatoa msimamo wao hadi sasa.

Muungano huo umekuwa ukisisitiza kuwa lazima Bw Odinga ajiunge nao kama kinara mwenzao, wala si katika hali ambapo anaonekana kuwa kiongozi wao.

Vile vile, wanadaiwa kushikilia sharti Bw Odinga awe tayari kumuunga mkono mmoja wao kuwa mgombea urais, kwani walimuunga mkono mnamo 2013 na 2017.

Katika hatua inayoonekana kurusha ndoano yake ya kisiasa katika ukanda wa Mlima Kenya, Bw Odinga alisema yuko tayari kushirikiana kisiasa na eneo hilo, hata ikiwa itamaanisha kumteua mmoja wao kuwa mgombea-mwenza wake.

Alisema tayari ameanza mazungumzo kuhusu hilo na jumbe mbalimbali ambazo zimekuwa zikimtembelea kwake kutoka ukanda huo.

“Nina uhusiano wa muda mrefu na wenyeji wa Mlima Kenya. Wao ni mashemeji wangu. Mwanangu wa kwanza, marehemu Fidel Odinga, alikuwa ameoa kutoka Kaunti ya Kiambu. Kakake mdogo Fidel, Raila Odinga Junior, ametoa mkewe katika Kaunti ya Murang’a. Hilo linaonyesha kuwa kando na kushirikiana, tu’ ndugu na jamaa wa karibu,” akasema Bw Odinga.

Alirejelea urafiki kati ya Mzee Jomo Kenyatta na babake, marehemu Jaramogi Oginga Odinga, akiutaja kuweka msingi katika ukaribu wake na eneo hilo.

Bw Odinga alipuuza dhana kwamba analichukia eneo hilo na hofu ambayo imekuwepo miongoni mwa baadhi ya wenyeji kuwa huenda akalipiza kisasi ikiwa atachukua uongozi.

“Hizo ni propaganda ambazo zimekuwa zikienezwa na wakosoaji wangu. Nimekuwa na uhusiano wa muda mrefu na viongozi kutoka Mlima Kenya tangu miaka ya themanini. Kwenye harakati za kupigania ukombozi wa pili, tulishirikiana na marehemu Stanley Matiba na mwenzake Charles Rubia. Vile vile, tuliongoza Serikali ya Muungano na Rais Mstaafu Mwai Kibaki kati ya 2008 na 2013,” akasema.

Alieleza aliwateua viongozi kama Bi Rachael Shebesh, Seneta Isaac Mwaura na Bi Mumbi Ng’aru kuhudumu kama wabunge maalum hapo awali “kutokana na ukaribu alio nao na eneo hilo.”

Hapo jana Ijumaa, Bw Odinga aliendelea kumkabili vikali Naibu Rais William Ruto, akimshauri kujiuzulu serikalini ikiwa anahisi haridhiki.

Alisema ni unafiki kwa Dkt Ruto kuendelea kupokea mshahara na marupurupu kutoka kwa serikali anayohisi imemtenga na hayuko sehemu yake tena.

Hilo linafuatia malalamishi ya Dkt Ruto kwamba ametengwa na majukumu yake kuchukuliwa na Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i.

“Wakati babangu (Jaramogi) alihisi hangeendelea kuwa makamu wa rais wa Mzee Kenyatta, alimwandikia barua na kujiuzulu rasmi wadhifa wake. Dkt Ruto anapaswa kuzingatia mfano huo,” akaeleza.

Wakati huo huo, alijitetea dhidi ya madai ya kuvuruga serikali, kufuatia handisheki kati yake na Rais Kenyatta.

Alisema huwa hapokei mshahara wowote kutoka kwa serikali, ispokuwa tu marupuru ya kustaafu.

“Ikiwa ningekuwa nimejiunga na serikali, basi washirika wangu wangekuwa wameteuliwa kuhudumu kwenye nyadhifa mbalimbali,” akaeleza.

Kauli yake inafuatia malalamishi ya Dkt Ruto na washirika wake kuwa Bw Odinga “aliivamia” serikali na kuvuruga mipango yote ya maendeleo ya serikali ya Jubilee.

You can share this post!

Ruto ataka majibu kuhusu ulinzi wake

Baadhi ya wanasoka wa haiba kubwa waliowahi kuondoka katika...