Michezo

Sijaagana na Gor Mahia licha ya hali kuwa tete – Kipkirui

August 25th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI matata wa Gor Mahia, Nicholas Kipkirui amefutilia mbali tetesi kwamba ameagana rasmi na mabingwa hao mara 19 wa Ligi Kuu ya humu nchini.

Nyota huyo wa zamani wa Zoo Kericho anakana madai hayo siku moja baada ya kufichuka kwamba yeye na wenzake Philemon Otieno na Jackson Owusu wa Ghana wamekatiza uhusiano na Gor Mahia kwa sababu ya kutolipwa mshahara kwa miezi minne iliyopita.

Uchechefu wa fedha kambini mwa Gor Mahia umeshuhudia miamba hao wakikatiza uhusiano na wanasoka wao wa haiba kubwa tangu muhula huu wa uhamisho wa wachezaji ufunguliwe rasmi.

Kati ya masogora tegemeo ambao wameondoka kambini mwa Gor Mahia kufikia sasa ni naibu nahodha Joash Onyango aliyetua Tanzania kuvalia jezi za mabingwa Simba SC na mvamizi Boniface Omondi aliyesajiliwa na mabwanyenye Wazito FC.

Wengine ni kipa chaguo la tatu Peter Odhiambo na Watanzania Dickson Ambundo (beki) na David Mapigano (mlinda-lango).

Kipkirui ambaye aliingia katika sajili rasmi ya Gor Mahia mnamo 2018, amesema angali na mwaka mmoja katika mkataba wake wa sasa na Gor Mahia.

Japo amefichua kwamba matamanio yake ni kusalia kambini mwa Gor Mahia, amedokeza kuhusu uwezekano wa kuagana rasmi na kikosi hicho cha kocha Steven Polack kwa kufuata taratibu zote zilizopo iwapo atapokea ofa nzuri zaidi.

“Sijabanduka Gor Mahia, sijakubali ofa yoyote nyingine kwingineko na waajiri wangu wa sasa hawajanipa barua ya kuniruhusu kuondoka. Ningali na mwaka mmoja kwenye mkataba wangu wa sasa ingawa zipo ofa tele ninazoendelea kupiga msasa,” akasema nyota huyo wa Harambee Stars.

Kwa mujibu wa Kipkirui, hali ya kifedha kambini mwa Gor Mahia ilisalia tete tangu waliokuwa wadhamini wao SportPesa wajiondoe kwenye soko la humu nchini.

“Wengi wa wachezaji wanakabiliwa na matatizo makubwa ya kifedha. Tumesalia kutegemea misaada ya wahisani na mashabiki,” akalalamika Kipkirui.

Udhamini wa Sh55 milioni ambao Gor Mahia walipata kutoka kwa kampuni ya mchezo wa kamari wa Betsafe mnamo Juni 2020 unatarajiwa kutolewa rasmi pindi kampeni za msimu mpya wa 2020-21 kwenye soka ya humu nchini zitakapoanza.

“Hali ni ngumu hasa ikizingatiwa kwamba wachezaji hawajalipwa kwa miezi kadhaa sasa. Itakuwa vyema kwa usimamizi kuingilia kati na kuokoa hali kabla ya wapinzani na vikosi vinginevyo nje ya Kenya kuchuma nafuu kutokana na hali tete ya sasa kambini mwa Gor Mahia na kutwaa wanasoka wote wa haiba kubwa,” akaonya Kipkirui.