Habari Mseto

Sijaagiza Punjani ashikwe, aache kubabaika – Haji

September 7th, 2019 1 min read

Na STEPHEN ODUOR

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma, Noordin Haji, amesema kuwa hajatoa kibali cha kumkamata mfanyabiashara tajiri wa Mombasa, Ali Punjani.

Akizungumza Ijumaa akiwa mjini Hola, Bw Haji alisema kuwa afisi yake haikuwa imetoa kibali cha kumtia nguvuni mwanabiashara huyo na ameingiwa na kiwewe bila sababu hadi akaomba msaada kortini.

“Hatujaonyesha sababu yoyote ya kumtia nguvuni Punjani ila tunafahamu kuwa ametafuta dhamana ili kuzuia kukamata, nakala ambazo hatujazipokea kufikia sasa,” alisema.

Hata hivyo, Bw Haji alisema kuwa afisi yake inapinga dhamana kama hizo kwa sababu zinahujumu michakato ya kukabiliana na uhalifu.

Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai alitangaza kuwa idara ya polisi ilikusudia kukaza kamba vita dhidi ya makundi ya uhalifu eneo la pwani na kuongeza juhudi za kuwanasa walanguzi wa mihadarati nchini.

‘Joto kali laja’

Bw Mutyambai alisema kuwa tayari kundi la vijana la Wakali Kwanza lilikuwa linahama mji wa Mombasa, huku akiwahakikishia kuwa walanguzi wa dawa za kulevya na hata watumiaji hawatastahimili joto linalokuja.

Alisema kuwa awamu ya pili ya msako dhidi ya walanguzi wakuu nchini halitasaza yeyote wakiwemo maafisa wa serikali bila kujali vyeo vyao.

“Mambo hayatakuwa rahisi hapa siku chache zijazo, inaelekea kuwa zaidi ya tulivyoanza zoezi la kwanza,” alisema.

Hapo jana, Bw Hillary Mutyambai alizuru kaunti ya Tana River kufahamiana na maafisa wa polisi na maeneo yao ya kazi.

Aliandamana na Bw Haji, Mwenyekiti wa Tume ya polisi Bw Eliud Kinuthia na mwenyekiti wa IPOA, Bi Anne Makori.