HabariSiasa

Sijaahidi Waiguru unaibu mwaka 2022 – Ruto

May 23rd, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

TANGAZO la Gavana wa Kirinyaga, Anne Mumbi Waiguru kuwa anaviziwa na mirengo miwili ya kisiasa awe mgombea mwenza 2022 ambalo vyombo vingi vya habari viliangazia Jumatano limepuuzwa na Naibu Rais, Dkt William Ruto.

Dkt Ruto akiwa katika mahojiano ya moja kwa moja na kituo cha redio cha Kameme FM na kile cha runinga cha Kameme TV amesema Alhamisi kwamba “labda ameahidiwa na mwingine bali sio mimi.”

Huku ikitazamiwa kuwa ulingo wa kisiasa hadi sasa unadhibitiwa na mrengo wa Ruto na ule wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga, huenda wafuasi wa Waiguru sasa wachukulie kuwa watahamishwa kutoka Jubilee ambacho ndicho chama cha gavana huyo na Ruto kwa sasa.

Tayari, Bi Waiguru ambaye kwa sasa anakabiliana na mawimbi makali katika kaunti yake kutoka kwa upinzani wa mwakilishi wa wanawake wa
Kirinyaga, Wangui Ngirichi na pia wengine wa kumpinga wakimtaka akawanie ugavana mwaka 2022 katika Kaunti ya Nyandarua ambako hivi majuzi alitangaza kuwa amepata mume Kamotho Waiganjo.

Ruto amesema: “Akimenyana (Waiguru) afanikiwe ni sawa, akitarajia kupewa asahau.”

Lingine la kufahamu katika uchanganuzi wa kauli ya Waiguru ni kuwa hivi majuzi ameridhiana na Raila ambapo hata aliondoa kesi mahakamani ambayo alikuwa amewasilisha akiteta hatua ya Raila kumhusisha na ufisadi.

Pia, ameridhiana hadharani na Ruto ambaye pia wamekuwa katika malumbano makali kuhusu ufisadi, Ruto akimtakia Waiguru kifungo gerezani naye Waiguru akijibu mipigo kuwa mrengo wa Ruto ndio mfisadi ndani ya serikali.

“Ingawa  ninajua kuwa wanawake hapa nchini hujumuisha asilimia pengine hata zaidi ya 50 ya idadi yote ya Wakenya, nikijua vyema kuwa tuko na safari ndefu ya kuafikia usawa ndani ya uongozi wa kitaifa, mimi sijamwahidi mwanamke yeyote kuwa nitamteua kuwa mgombea mwenza,” amesema Ruto.

Amesema kuwa katika mawazo yake ya uwaniaji urais 2022, kila mtu atapambana katika kichungi cha demokrasia.

“Mimi nikimenyania ndani ya Jubilee kutafuta tiketi ya kuwa Rais naye Waiguru ajumuike ndani ya ushindani uo huo kumenyana apate wadhifa huo anaosema ameahidiwa,” amebainisha Ruto.

Dkt Ruto amesema kwamba ndani ya uwaniaji wa urais katika taswira ya siasa za sasa ni lazima kila mmoja ajitume kujipigia debe kwa wapigakura, akionya kuwa wakati wa kuketi katika afisi na kugawa vyeo “umepitwa na wakati”.

“Hii ndiyo sababu huwa natanga na njia kila kona ya nchi hii nikisaka ufuasi na nikiuza sera kwa kuwa mtihani wa 2022 utajumuisha sehemu ya usomi ambao ni wa kuunda sera, na ile ya uhalisia mashinani ambao ni kutangamana na uuzaji wa sera,” ameweka wazi.

Amemshauri Waiguru kuwa ikiwa analenga kuwa mgombea mwenza, basi la muhimu ni alivalie njuga suala hilo, ajipange kimikakati na katika meza ya kuunda mrengo na timu ya ushindi, awajibikie uwaniaji huo wake kupitia hesabu ya uhakika.

“Meza hiyo itaandaliwa hivi karibuni… Hatuko mbali na 2022. Uchaguzi unajulikana ni wa siku gani… Hapo katika kujipanga ajipenyeze na ajiwakilishe kama aliye na maono kwa Wakenya na pia aliye na uthabiti kisiasa… Akishinda nami nishinde tujipate pamoja kama mgombea wa urais naye mgombea mwenza basi tutawajibikia hilo kwa umoja unaostahili,” akasema.