Makala

'Sijafa moyo licha ya kupoteza ajira kipindi hiki cha janga la Covid-19'

September 13th, 2020 3 min read

Na SAMMY WAWERU

PURITY Wanjiru amesomea taaluma ya upishi na huduma za mikahawa na baada ya kufuzu miaka kadhaa iliyopita alipata kazi katika hoteli moja jijini Nairobi.

Amekuwa akihudumu kama mpishi, ambapo amebobea kuandaa vyakula tofauti, kuanzia vile vya kiasili na mapishi kwa njia ya kisasa.

Kusomea mapishi, ilikuwa taaluma ya chaguo lake la kwanza na iwapo asingeiwahi anasema angekumbatia kozi ya utalii. “Kimsingi, ninapenda mapishi. Uraibu ulianza tangu nikiwa mdogo,” Purity anasema.

Akiwa mzaliwa wa Nyeri, anaelezea kwamba alianza mapishi baada ya kufanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE.

Kenya ilipothibitisha kisa cha kwanza cha Covid-19 mnamo Machi 2020 mambo yalianza kuenda mrama.

Kazi aliyoipenda kwa dhati na iliyomkithi riziki na mahitaji mengine ya kimsingi ikaanza kuyumbishwa.

Kadri visa vya maambukizi ya corona vilizidi kuongezeka nchini, ndivyo mambo yaliendelea kuwa mabaya.

Uchumi ulianza kudorora, sekta mbalimbali zikaathirika kwa kiasi kikuu, ikiwemo ya biashara, mikahawa na utalii.

Ili kusaidia kuzuia kuenea kwa maambukizi, serikali iliweka sheria na mikakati maalum. Ni kanuni zinazosemekana kuathiri kwa kiwango kikubwa sekta ya mikahawa na utalii nchini, hoteli zikafungwa kwa muda.

Kufikia mwezi Aprili mambo yalikuwa yamezidi unga. Ni katika kipindi hicho ambapo Purity, 24, anasema alipoteza ajira.

“Tulisimamishwa kwa muda usiojulikana. Biashara iliathirika, kiasi cha wateja kukosekana,” mwanadada huyo anadokeza.

Kufikia sasa Purity anasema pamoja na wafanyakazi wenza hawajapata mwaliko wa kurejea tena kazini, licha ya sekta ya mikahawa kupata afueni kuanzia mwezi Mei.

Aidha, Wizara ya Afya iliruhusu kufunguliwa kwa hoteli na mikahawa ila kwa kuzingatia kanuni na mikakati.

Ni kanuni ambazo wengi wa wamiliki wa mikahawa wameshindwa kuafikia kufikia sasa. “Mkahawa niliokuwa nikifanya kazi eneo la Thika Road, mmiliki alishindwa kuafikia matakwa yanayohitajika kwa sababu ni bei ghali,” anasema Charity Muthoni, mhudumu na ambaye anaeleza kwamba hajakuwa kazini tangu Juni 2020.

“Imekuwa kibarua kulipa kodi ya nyumba jijini Nairobi. Nililazimika kupeleka watoto wangu mashambani,” anadokeza mama huyo wa watoto wawili.

Ili mikahawa na hoteli iruhusiwe kufunguliwa, inatakiwa kuwa na cheti kuonyesha imeafikia vigezo faafu kuonyesha iko mstari wa mbele katika kuzuia kuenea kwa virusi vya corona kuwalinda wafanyakazi na wateja.

Isitoshe, inapaswa kuwa na vifaa maalum vya kupima wateja kiwango cha joto, vifaa vya kunawa mikono na pia vitakasa mikono.

Wahudumu nao wanatakiwa kuwa na cheti cha Covid-19, kinachoonyesha hawana virusi.

Purity Wanjiru. Picha/ Sammy Waweru

Hali kadhalika, mpangilio wa viti na meza unatakiwa kuzingatia umbali kati ya mtu na mwenzako, hayo yakiwa mahitaji machache tu kuorodhesha. Kimsingi, ni kanuni ambazo wamiliki wa hoteli na mikahawa wanalalamikia kuwa ghali.

Michael Murimi ambaye alikuwa akihudumu kama mpishi katika mkahawa mmoja wa kifahari jijini Nairobi, anasema alipoteza nafasi yake ya kazi baada ya kufungiwa mashambani kufuatia zuio la kuingia na kutoka Nairobi lililodumu kati ya Aprili 6 – Julai 6.

“Nilikuwa nimenunua pikipiki awali na nimelazimika kuingilia huduma za bodaboda,”Murimi baba wa watoto watatu anadokeza.

Purity Wanjiru anaambia Taifa Jumapili kwamba kwa sasa anafanya kibarua chochote kinachojiri.

Awali, baada ya kupoteza kazi ya upishi, alipata nafasi katika mojawapo ya kampuni za bima nchini ila anasema ahadi za kulipwa mshahara ziligonga mwamba.

“Sijafa moyo, nina imani janga la Covid-19 ni la muda tu na litaisha. Kwa walioathirika kama mimi, muhimu ni kufanya vibarua vinavyopatikana hata ikiwa ni kufulia watu nguo, kuchuuza bidhaa za kula…Bora unaweza kuwekelea tonge la mlo mezani na kukithi mahitaji ya kimsingi,” Purity anashauri.

Mary Nderitu, mmiliki wa nyumba za kukodi Nairobi anasema athari za corona pia zimetatiza kwa kiasi kikuu biashara ya nyumba za kupangisha. “Wengi wamehamia mashambani kwa kushindwa kulipa kodi na kukithi familia zao riziki na mahitaji muhimu ya kimsingi,” Mary akasema wakati wa mahojiano.

Mama huyo hata hivyo anashauri watu kutobagua kazi, ikizingatiwa kuwa mengi ya mashirika na kampuni za kibinafsi zinaendelea kufuta wafanyakazi kwa kushindwa kuwalipa mishahara.

“Kwa mfano, ukianza kupikia watu chapati eneo unakoishi, utaweza kujiendeleza kimaisha. Covid-19 imetufunza mengi, ni muhimu kutathmini njia mbadala kusukuma gurudumu la maisha,” anahimiza.

Takwimu za hivi punde zinaonyesha watu 1.7 milioni walipoteza ajira kati ya mwezi Aprili na Juni, kulingana na Shirika la Takwimu Nchini, KNBS.

Katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita, idadi ya wanaothibitishwa kuambukizwa corona nchini imeonekana kushuka, japo Shirika la Afya Duniani limetoa tahadhari “watu wasipuuze mikakati iliyowekwa kusaidia kudhibiti maambukizi zaidi”.

Maelezo ya picha

Picha 1 – 4: Purity Wanjiru alikuwa mpishi katika mojawapo ya mikahawa jijini Naiorobi. Kufuatia athari za Covid-19, ni miongoni mwa waliopoteza ajira.

Picha 5 – 8: Wanjiru anasema kwa sasa anafanya vibarua vinavyoibuka ili kupata riziki.