Habari Mseto

Sijafika mahakamani kupinga kufunguliwa kwa shule – Omtatah

October 7th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MWANAHARAKATI Okiya Omtatah amepuuzilia mbali uvumi unaoenea mitandaoni kwamba amewasilisha kesi mahakamani kupinga kurejelewa kwa masomo ya kawaida kwa wanafunzi wa Gredi ya Nne, Darasa la Nane na Kidato cha Nne.

Kwenye taarifa aliyoitoa Jumatano Bw Omtata amewaambia Wakenya na wadau katika sekta ya elimu wakiwemo wazazi, kuchukulia habari hizo kama “feki”.

“Saa chache baada ya Waziri wa Elimu George Magoha kutangaza kuwa wanafunzi wa Gredi ya Nne, Darasa la Nane na Kidato cha Nne watahitajika kurejelea masomo kuanzia Jumatatu, habari zilienea mitandaoni kwamba nimeenda mahakamani kupinga hatua hiyo. Hizi ni habari za uwongo na ninaomba Wakenya kuzichukulia kama habari feki,” akasema.

Wazazi wengi waliiingiwa na wasiwasi baada ya habari kuibuka kuwa Bw Omtatah amewasilisha kesi mahakamani kupinga kufunguliwa kwa shule kwa msingi kuwa wazazi hawako tayari.

Kando na kutangaza kurejelewa kwa masomo, waziri Magoha pia alitangaza tarehe mpya ambapo mitihani ya kitaifa itafanyika.

Kulingana na taarifa hiyo mtihani wa KCPE itaanza mnamo Machi 22, 2021, na kumalizika mnamo Machi 24, 2021.

Mtihani wa kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) nao utaanza mnamo Machi 3, 2021, na kumalizika mnamo Aprili 4, 2021.

Duru pia zinasema kuwa wanafunzi wa Gredi ya Tatu, Darasa la Saba na Kidato cha Tatu huenda wakarejea mnamo Oktoba 18, 2020, uamuzi ambao utatolewa kutegemea na hali ya Covid-19 nchini.