Habari MsetoSiasa

Sijajiuzulu lakini maisha yangu yako hatarini – Moses Kuria

January 10th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Gatundu Kusini Moses Kuria amekanusha madai kwamba amejiuzulu wadhifa wake wa ubunge huku akidai kuwa maisha yake yamo hatarini.

Akihutubia  wanahabari katika majengo ya bunge Alhamisi Bw Kuria alisema kuwa amewasilisha ripoti kuhusu vitisho dhidi ya maisha yake kwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti.

“Hawa watu ambao wanaeneza habari za uwongo kuwa nimejiuzulu ndio wamekuwa wakitishia maisha yangu kwa msingi kuwa nilikosea heshima rais Uhuru Kenyatta kufuatia kauli yangu iliyofasiri vibaya kuashiria kuwa eneo la Mlima Kenya limetengwa kimaendeleo,” akasema Bw Kuria.

“Vyombo vya habari vilivyoripoti kwamba nimejiuzulu vinapasa kujitayarisha kujitetea kortini. Nitaomba nilipwe ridhaa,” akaongeza.

Gazeti la The Star lilikuwa limeripoti katika tovuti yake kwamba Bw Kuria amemwandikia barua Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi akifahamisha rasmi kuhusu kujiuzulu kwake.

Mbunge huyo wa chama cha Jubilee vile alionekana kukunja mkia kufuatia madai yake kwamba Rais Uhuru Kenyatta hajatekeleza miradi ya maendeleo katika eneo la Mlima Kenyatta.

Huku akimwomba msamaha Rais kwa mara ya pili, alisema anaunga mkono azma kiongozi wa taifa ya kuanzisha miradi ya maendeleo katika maeneo mengine ya nchi.

“Namwomba msamaha Rais Kenyatta kwa mara nyingine kwa hukerwa na dhana mbaya iliyotokana na matamshi yangu. Nimefafanua hapo awali kwamba kauli yangu haikumlenga Mheshimiwa Rais bali viongozi wa Kiambu ambao wamekuwa wakizembea kazini,” akasema.

Bw Kuria pia alisema anaunga mkono Muafaka wa Maridhiano kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga akisema amefaidi pakubwa kutokana kwayo.

“Binafsi nimefaidi zaidi kutokana na handisheki kwa sababu sasa ninaweza kuzuri kaunti za Homa Bay, Kisumu na Siaya bila shida yoyote. Hapo zamani mwisho wa safari yangu mjini Kisumu ulikuwa uwanja wa ndege wa Kisumu lakini sasa naweza kutangamana na wananchi bila shida yoyote,” akasema.

Bw Kuria alisema amemwalika Bw Odinga katika eneo bunge la kuzindua miradi ya maendeleo kwa moyo wa Muafaka wa Maridhiano.

Hata hivyo, hakutaja ni lini Bw Odinga atazuru eneo hilo la Gatundu Kusini.