Sijali kupigwa kalamu, afoka Kang’ata

Sijali kupigwa kalamu, afoka Kang’ata

Na CHARLES WASONGA

KIRANJA wa Wengi katika Seneti Irungu Kang’ata amesema kuwa yuko tayari kupokonywa wadhifa wake katika bunge hilo kutokana na msimamo wake kwamba mchakato wa BBI sio maarufu katika eneo la Mlima Kenya.

Akiongea na Taifa Leo Dijitali katika majengo ya bunge Jumatatu, Bw Kang’ata alisema changamoto zinazoikabili BBI katika eneo hilo zinapasa kutatuliwa ili kuokoa serikali kutoka na “aibu” endapo wakazi wa Mlima Kenya watakataa mswada wa mageuzi ya Katiba.

“Kwa mfano, ajenda ya mageuzi ya Katiba kupitia BBI katika eneo la Mlima Kenya inapasa kuendeshwa na viongozi waliochaguliwa wala sio maafisa wa utawala wa mkoa kama inavyofanyika wakati huu. Hali ikiendelea hivi huenda serikali ikaaibishwa wakati wa kura ya maamuzi ikizingatiwa kuwa Rais Kenyatta anatoka eneo hilo,” akasema.

“Huu ndio msimamo wangu pamoja na masuala yote ambayo niliyaeleza katika barua yangu kwa Rais. Sijutii msimamo huu hata kama utanigharimu wadhifa wangu kama Kiranja wa Seneti, kazi ambayo nimeitekeleza kwa uadilifu kwa miezi sita iliyopita,” akaongeza seneta huyo wa Murang’a.

Vile vile, Kiranja huyo wa Wengi alionekena kuongezea zaidi mgawanyiko ndani ya Jubilee alipounga mkono wazo la Naibu Rais William Ruto kwamba wapiga kura waruhusiwe kupiga kura kwa zaidi ya maswali mawili katika kura ya maamuzi kuhusu mswada wa BBI.

“Jambo halifai kupingwa kwa misingi ya yule aliyelitoa. Linapasa kuchanganuliwa kwa uwazi kubaini uzuri au ubaya wake kwa njia huru bila kuingizwa siasa. Hii ndio maana naunga mkono wazo la Dkt Ruto kwamba Wakenya wapewe nafasi ya kupigia kura masuala mbalimbali katika BBI ili tusipoteza mazuri yaliyomo kwenye mswada huo kupitia kura ya NDIO au LA,” Bw Kang’ata akaongeza.

Baada ya barua yake kwa Rais Kenyatta kufichuliwa katika vyombo vya habari wiki jana, wanasiasa kadhaa wandani wa Rais Kenyatta wamemshutumu Seneta huyo wakidai “anapanga kurejea katika kambi ya Tangatanga ili kufanikisha ndoto yake ya kuwa Gavana wa Murang’a 2022.”

Hata hivyo, Jumatatu Bw Kang’ata alipuuzilia mbali madai hayo akishikilia kuwa ataendelea kuwa mwaminifu kwa serikali, Rais Kenyatta na chama chake cha Jubilee.

“Nitaendelea kuwa mwaminifu kwa serikali na kuendelea kutekeleza wajibu wangu wa kusema ukweli. Kwa hivyo, haina maana kwa viongozi wenzangu kama vile Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Amos Kimunya na Ngunjiri Wambugu (Mbunge wa Nyeri) kunirushia matusi yasiyo na maana yoyote,” akasema.

You can share this post!

Wenyeji watawala mbio za Great Ethiopian Run, Wakenya...

Kitendawili cha barakoa