Habari Mseto

Sijatangaza sitamuunga mkono Ruto 2022 – Uhuru

November 16th, 2019 2 min read

Na JOSEPH WANGUI

RAIS Uhuru Kenyatta aliwazima viongozi kutoka eneo la Mlima Kenya ambao wamekuwa wakidai kuwa amekiuka ahadi yake kwa Naibu Rais William Ruto akisema katika mkutano wa Ijumaa kwamba hajawahi kusema hatamuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Rais aliyekutana na viongozi wa eneo la Mlima Kenya katika ikulu ndogo ya Sagana, Kaunti ya Nyeri, aliwaambia wabunge hao waache kumkumbusha kila mara kwamba, aliahidi kumuunga mkono Dkt Ruto kwenye uchaguzi mkuu ujao. Chama cha Jubilee kimegawanyika katika mirengo miwili; ‘Tangatanga’ unaomuunga Dkt Ruto na kupinga handisheki kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga na ‘Kieleweke’ unaounga handisheki na kupinga azma ya Dkt Ruto kugombea urais.

Inasemekana Rais Kenyatta alishangazwa na mirengo hiyo akisema hajawahi kusema kwamba hatamuunga Dkt Ruto au kwamba anaunga Bw Odinga.

Wabunge wanaomuunga Naibu Rais wamekuwa wakidai muafaka kati ya Rais Kenyatta na Raila Odinga unalenga kuzima azma ya Dkt Ruto ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Rais aliwaambia viongozi hao kwamba, kuridhiana na Bw Odinga hakufai kuchukuliwa kuwa anamuidhinisha kuwa mrithi wake.

Akihutubu kwa lugha ya Kikuyu, Rais aliwaeleza viongozi hao kwamba handisheki yake na Bw Odinga haimaanishi anaunga azima yake ya kugombea urais.

Kuhusu ripoti ya BBI

Kuhuru ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI), Rais Kenyatta aliwaambia viongozi wa Mlima Kenya wakome kushuku yaliyomo akisema hata yeye hajaiona.

Aliwachekesha waliohudhuria aliposema kwamba alilazimika kumpigia simu mwanachama mmoja wa jopo hilo na kumuuliza iwapo walikuwa wamewapa wanasiasa nakala ya ripoti kabla ya kumkabidhi rasmi.

Rais Kenyatta aliwahakikishia kuwa ripoti hiyo itachapishwa na nakala kusambaziwa Wakenya wasome na kutoa mapendekezo.

Hata hivyo, alisema anatarajia itashughulikia masuala ya ushirikishi, kumaliza ghasia za baada ya uchaguzi na usawa katika ugavi wa rasilmali.

Baada ya mkutano huo, viongozi walitoa hisia tofauti baadhi wakifurahi rais aliwahimiza kuzingatia maendeleo badala ya siasa za 2022.

Mbunge wa Nyeri Mjini, Ngunjiri Wambugu alisema uamuzi wa rais kufafanulia viongozi kutoka ngome yake maana ya handisheki utatuliza wasiwasi kwamba inahusu siasa za 2022.

“Tumefurahi alieleza kwamba handisheki yake na Raila haikumaanisha alimuidhinisha kugombea urais. Rais alieleza ni kwa sababu ya handisheki Jubilee iliweza kusimamisha mgombeaji kwenye uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra,” alisema Bw Wambugu.

Wanahabari hawakuruhusiwa kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na zaidi ya viongozi 4000 kutoka kaunti 10 za eneo la Mlima Kenya.