Habari Mseto

'Sijuti kamwe kukataa nyumba ya bure kutoka kwa Uhuru'

February 27th, 2019 2 min read

NA FRANCIS MUREITHI

MAMA anayedaiwa alikataa kupokea nyumba aliyokabidhiwa na Rais Uhuru Kenyatta, amesema hajutii uamuzi huo hata baada ya makazi hayo kukabidhiwa familia nyingine.

Bi Damaris Wambui Kamau, mamake Dennis Ngaruiya aliyemtumbuiza Rais wakati wa sherehe za wanajeshi kwenye Ikulu ya Nairobi amesema hajishughulishi tena na suala hilo wala hana chuki na familia hiyo.

Bi Kamau mwenye umri wa miaka 60, pia alikana kuwa kukataa zawadi hiyo ni ishara ya kutoonyesha shukrani kwa kiongozi wa nchi, huku akiwataja wanaosema hivyo kama wasioelewa utata unaohusu nyumba aliyoikataa.

Taifa Leo ilipomtembelea katika nyumba yake ya udongo, mtaa wa Lanet, alionekana kutotikiswa na uamuzi wake. Alielezea kuwa na imani kwa Maulana, na kusisitiza kwamba nyumba aliyopewa haikuwa ile Rais Kenyatta alikusudia apokezwe.

“Nimewacha kila kitu mkononi mwa Mwenyezi mungu na ipo siku ukweli utabainika. Iwapo baraka za mwanangu wa kiume Dennis zililenga kunufaisha familia nyingine, basi iwe hivyo na sina kinyongo na hilo,” alisema Bi Kamau ambaye ni mama wa watoto sita.

Aliongeza, “ Nafahamu baraka za Mungu ni nyingi na ipo siku atatuzawidi, nimeamua kuendelea na maisha yangu.”

Katika mahojiano hayo alituonyesha picha ambazo zimesalia kama kumbukumbu ya siku aliyodhania ingemfungulia milango ya heri maishani.

Hata hivyo, ingawaje anaeleza hajuti kuikataa, anayo majonzi .

Alisimulia jinsi mambo yalivyofanyika tangu siku alipoingia Ikulu baada ya mwanawe kumchekesha Rais kwa tumbuizo la kipekee, namna Rais Kenyatta alivyoelekeza maafisa wa Ikulu kuhakikisha kwamba masomo ya mwanawe yamefadhiliwa hadi Chuo Kikuu, na makazi mazuri ambayo sasa yamezua utata na kuvutia umma.

“Kile nafahamu ni kwamba mambo yangu na mwanangu yatasalia mazuri kwa mapenzi ya Mungu. Maafisa wa Ikulu wanaweza kutuhangaisha lakini Mungu aliye juu mbinguni anawajali wajane na maskini kama sisi kuliko wao,” alisema.

“Iwapo zawadi kutoka kwa Rais ililenga kumfaa mtu mwingine mwenye mahitaji muhimu kutuliko jinsi wanavyowahadaa Wakenya, basi sina ugomvi nao kwasababu naamini ukweli utajulikana siku moja.”