Habari za Kitaifa

Siko vizuri sana na Rais, lakini tutasuluhisha mambo, Gachagua sasa aungama


NAIBU wa Rais Rigathi Gachagua ameashiria waziwazi kwa mara ya kwanza kabisa kwamba hayuko vizuri na mkubwa wake, Rais William Ruto.

Bw Gachagua, hata hivyo, alisema tofauti zilizopo baina yake na Rais Ruto zitashughulikiwa kwa ajili ya maendeleo, umoja na demokrasia.

Malumbano ndani ya Kenya Kwanza, alisema Bw Gachagua Jumapili, yalikuwa yanachongewa na watu aliosema waliingia serikalini hivi majuzi na ambao alisema wameteka ajenda ya serikali na kutupa nje watu ambao wamesimama na Dkt Ruto kwa dhiki na faraja.

Katika hatua ambayo iliendelea kuonyesha jinsi wawili hao hawapatani tena, Bw Gachagua alisema atazungumza kivyake na vijana wa Gen Z ambao wamekuwa wakifanya maandamano, kando na mchakato jumuishi wa wawakilishi 100 aliotangaza Rais Ruto.

Aidha, Bw Gachagua aliahidi masuala yanayosababisha tofauti baina yake na Rais Ruto yatatuliwa hivi karibuni.

Akiongea Jumapili katika Kanisa la Deliverance mjini Bomet alikohudhuria ibada na mchango, Bw Gachagua alisema kuwa masuala ya Gen-Zs ni mazito na yanahusu uongozi wa taifa hili.

“Hii ndio maana nitawaita hao vijana tuzungumze ili tusuluhishe malalamishi yao yanayochangia wao kufanya maandamano yanayoingiliwa na wakora na kusababisha maafa,” Bw Gachagua akaeleza.

Mnamo Jumamosi Rais Ruto alitangaza kubuniwa kwa Kamati shirikishi itakayoongoza mazungumo kujadili masuala yaliyoibuliwa na vijana wa Gen-Z na yaliyochangia wao kuandamana kote nchini mnamo Jumanne.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei, kamati hiyo itajadili masuala kama vile ukosefu wa ajira, mzigo wa madeni ya Kenya, kero la ufisadi, miongoni mwa masuala mengine.

Jana, Bw Gachagua aliwashauri viongozi waliochaguliwa kukoma kuwapuuza Wakenya waliowachagua katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Aidha, Bw Gachagua aliwataka maafisa wa serikali kusikiza masuala yanayoibuliwa na wananchi haswa katika nyanja za kiuchumi na kisiasa.

“Wananchi ndio wadau wakuu katika masuala ya uongozi ambayo viongozi wanapania kushughulikia wakati kama huu ambapo taifa linakumbwa na misukosuko. Kwa hivyo, wanafaa kusikizwa.” Akasema.

Bw Gachagua akaongeza: “Tukome kuwatapikia watu waliotuchagua. Tusiwaonyeshe majigambo na ukaidi kwa mising kwamba baadhi yetu tuko na pesa na mamlaka,” Bw Gachagua akasema.