Siku mbili zatenganisha kifo cha mwanamuziki Albert Gacheru wa Maitu na cha kaka yake mkubwa

Siku mbili zatenganisha kifo cha mwanamuziki Albert Gacheru wa Maitu na cha kaka yake mkubwa

Na MWANGI MUIRURI

SIKU mbili tu baada ya mwanamuziki maarufu eneo la Mlima Kenya Albert Gacheru Wa Maitu kuaga dunia akiwa na umri wa miaka 59, kaka yake mkubwa naye amefariki akiwa na umri wa miaka 69.

Bw Wa Maitu alifariki katika hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) baada ya kusemwa kuugua nimonia huku nduguye akifahamika kama Basilio Ngunjiri Kiarie naye akifariki katika hospitali ya JM Memorial iliyoko mtaani Olkalou, Kaunti ya Nyandarua “baada ya kuugua kwa muda mfupi na kulazwa.”

Kwa mujibu wa ndugu yao mdogo kwa jina Julius Kanyora, ni siku mbili za wingu la simanzi lakini “tumekubali uamuzi wa Mungu ambaye ndiye mwenye umiliki wa uhai wetu.”

Marehemu Wa Maitu atakumbukwa vyema kwa ngoma zake mbili miongoni mwa nyingi nyinginezo. Nazo ni ‘Mumunya’ (Busu) na ‘Mwendwa wakwa Mariru’ (Ewe Kipenzi Changu Unang’aa Ajabu).

Albert Gacheru. Picha/ Maktaba

Pia atakumbukwa kwa harakati zake za kupambana na wezi wa hakimiliki za sekta ya muziki.

Kwa upande wake Bw Ngunjiri, alikuwa mwalimu mstaafu na ambaye alikuwa amewekeza katika biashara ya duka la ujumla likifahamika kama BN Enterprises.

Mwendazake Ngunjiri amemuacha mjane na watoto sita ambapo wawili ni wa mke wake wa kwanza aliyeaga dunia miaka 15 iliyopita.

Bw Kanyora amesema kuwa kwa sasa familia imezindua mipango ya mazishi na ambayo huenda ifanyike Jumamosi ijayo.

“Tulikuwa tumeafikia asilimia 80 ya maandalizi ya mazishi ya Bw Wa Maitu. Tunawazia kuunganisha mazishi yao wawili na tuwape heshima zao za mwisho siku moja ikiwa ni Jumamosi ijayo,” akasema Bw Ngunjiri.

Ushirika wa Wanamuziki na Watunzi hapa nchini—Talented Musicians and Composers (Tamco) Sacco—chini ya mwenyekiti wao Bw Epha Maina umetoa salamu za pole na rambirambi kwa familia hii.

“Ni huzuni kuu lakini tufanye nini? Mungu aliyetujalia uhai wao ndiye ameamua kuwachukua… Hata sisi tuko katika mkondo huo wa kusafiri huko na tunalobakia nalo kwa sasa ni kumtegemea Mungu atupe nguvu za kustahimili yaliyotokea,” akasema Bw Maina.

Bw Maina amesema kuwa ushirika wake utaungana na familia hii kwa hali na mali “huku la mno tukiiombea Mungu iwape nguvu na imani ya kimaisha kwamba tuliobaki nyuma ndio sasa tunafaa kuzingatia yale maazimio mema wendazao walikuwa wakilenga kuafikia ili tuyatimize kwa niaba yao.”

You can share this post!

Mwanamume mpenda sketi ashtakiwa kwa ubakaji

UHURUTO WALIVYOFUTA REKODI YA KIBAKI