Siku Mudavadi, Kalonzo ‘walitekwa nyara’ na wanakijiji

Siku Mudavadi, Kalonzo ‘walitekwa nyara’ na wanakijiji

Na LEONARD ONYANGO

VINARA wa One Kenya Alliance (OKA) sasa wanadai walitekwa nyara na kulazimishwa kuchangia fedha za matibabu kwa mgonjwa wa saratani katika Kaunti ya Trans Nzoia, wiki iliyopita.

Kiongozi wa Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi na mwenzake wa Wiper, Kalonzo Musyoka, wikendi walisema hali ngumu ya maisha imelazimu Wakenya ‘kuteka nyara’ wanasiasa ili kupata fedha za matibabu na mahitaji mengine ya kimsingi.

“Tulikuwa barabarani katika Kaunti ya Trans Nzoia na tulipofika mahali fulani tulitekwa nyara na kulazimishwa tusaidie aliyekuwa mchezaji wa soka wa timu ya Sofapaka anayeugua saratani.“Kutokana na hali ngumu ya maisha, Wakenya wamefikia kiwango cha kuteka nyara watu barabarani wakisema ni lazima mchange kidogo tupeleke mtu hospitalini.

Hiyo ni dalili ya kuonyesha kuwa tuko katika hali ya hatari,” akasema Bw Mudavadi.Viongozi hao walikuwa wakirejelea kisa cha Novemba 27, mwaka huu, ambapo vijana waliokuwa na mabango walitatiza mkutano wao wa kisiasa mjini Kitale.

Vijana hao waliwataka viongozi hao wa OKA wamsaidie mchezaji wa klabu ya Sofapaka, Wisdom Naya, anayehitaji Sh2.5 milioni kwenda kutibiwa nchini India.Vijana hao wenye mabango walitatiza hotuba ya viongozi wa OKA kwa dakika kadhaa na juhudi za mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa kuwatuliza ziliambulia patupu.

Seneta wa Kakamega, Cleophas Malala alilazimika kusitisha siasa na badala yake kuwataka kinara wa Ford Kenya Moses Wetang’ula na Bw Mudavadi kuzungumzia suala la Wisdom.Bw Wetang’ula alisimama na kuahidi kuwa viongozi wa OKA watatoa jumla ya Sh500,000 kusaidia mchezaji huyo.

Vijana waliokuwa na mabango, hata hivyo, hawakuridhishwa na kiasi hicho na wakaendelea kupiga kelele – hatua iliyomfanya Bw Wetang’ula kufoka vikali.“Msitupatie masharti, mnasumbuliwa na nini?” akafoka Bw Wetang’ula.Ilibidi Bw Mudavadi aingilie kati na kuchukua moja ya mabango hayo na kuwataka Wakenya kumsaidia mchezaji huyo.

“Ninashika bango hili ili vituo vyote vya televisheni vione ili Wisdom apate usaidizi si kutoka tu kwetu sisi (OKA) bali Wakenya wote ili atibiwe na kupona na arudi kucheza mpira.“Wasamaria wema wanaweza kutuma mchango wao kwa paybill:

8043369 ili Wisdom aende kutibiwa,” akasema Bw Mudavadi.Naye kiongozi wa Ford Kenya aliahidi kutumia kituo chake cha redio na runinga; Nyota FM na Nyota TV mtawalia, kuwasihi Wakenya kila siku kumpa msaada mchezaji huyo.

Kinara huyo wa ANC alitumia fursa hiyo kujipigia debe kuwa iwapo atachaguliwa kuwa rais, atahakikisha kuwa Kenya inakuwa na hospitali zenye vifaa vya kisasa za kutibu saratani.“Sisi tulikuja hapa kupiga siasa lakini tumetatizwa na suala hili la Wisdom.

Huu ni ujumbe kwamba suala la matibabu humu nchini lingali changamoto kubwa,” akasema Bw Mudavadi.

You can share this post!

Kaunti yatishia kushtaki Wizara ya Utalii kwa Rais

Jaribio la kupiga breki Wapwani KPA lazua joto

T L