Habari

Siku ya Chakula Duniani: Kenya ingali inakabiliwa na ukosefu wa chakula cha kutosha

October 16th, 2019 2 min read

Na MAGDALENE WANJA na BARNABAS BII

HUKU ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Chakula Duniani – World Food Day – leo Jumatano, Kenya ni mojawapo ya nchi ambazo zinaendelea kukabiliana na tatizo la njaa.

Kufikia Julai 2019, zaidi ya Wakenya 2 milioni walikuwa wanakabiliwa na ukosefu wa chakula.

Hii ni licha ya Kenya kutegemea ukulima kwa njia kubwa zaidi kujikimu kiuchumi.

Ukulima huchangia katika uchumi wa nchi kwa kiwango cha asilimia 24.

Kulingana na ripoti ya mwaka 2019 ya Taasisi ya Masomo ya Usalama – Institute for Security Studies – ili kufikia hatua ya kuwa na hakikisho la chakula cha kutosha kufikia mwaka 2030, iitahitajika kuongezea mapato na mavuno ya chakula kwa asilimia 75.

“Wakenya 3.4 milioni wameathirika na makali ya njaa kwa kiwango kikubwa ambapo 309,000 wamelazimika kuhama kutoka kwa makazi yao kutokana na njaa,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Kaunti zilizoathirika zaidi ni zile za Marsabit na Turkana.

Mada kuu ya mwaka 2019 ni ‘Vitendo Vyetu Ndiyo Mustakabali Wetu: Lishe Bora kwa Dunia Isiyo na Njaa’ yaani kwa Kiingereza ‘Our Actions Are Our Future, Healthy Diets for A #ZeroHunger World’.

Bei ya mahindi

Haya yanajiri huku tayari bei ya unga wa mahindi ikitarajiwa kupanda tena baada ya wasagaji kumaliza magunia milioni 1.9 ya mahindi ambayo yalitolewa na serikali kwa bei nafuu Septemba 2019.

Hali imeharibiwa zaidi na kupungua kwa uagizaji mahindi kutoka Uganda na Tanzania.

“Uhaba wa mahindi nchini pamoja na upungufu wa uagizaji kutoka Uganda na Tanzania umefanya bei ya mahindi kupanda. Jinsi ilivyo kwa sasa, hatutakuwa na budi ila kupandisha bei ya unga,” akasema Bw David Kosgey, mmoja wa wasagaji mahindi mjini Eldoret.

Kiwango cha mahindi kinachoingizwa kutoka Uganda kimepungua katika muda wa miezi miwili iliyopita na kufanya gunia la kilo 90 kuuzwa kwa Sh3,200 kutoka Sh2,800.

Mahindi kutoka Tanzania yanauzwa kwa Sh3,400 kutoka Sh3,000 kwa kila gunia la kilo 90. Kulingana na Baraza la Nafaka Afrika Mashariki (EAGC), uhaba wa mvua unaweza kufanya mavuno ya mahindi kupungua Uganda, Tanzania na Kenya na hivyo basi kusababisha bei ya unga kupanda zaidi.