Habari Mseto

SIKU YA KIMATAIFA YA MTOTO WA KIAFRIKA: Jamii na wazazi wahimizwa kuhakikisha watoto wako salama

June 16th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

HUKU Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kiafrika ikiadhimishwa leo Jumanne, afisa mkuu wa watoto mjini Mombasa Bw Philip Nzenge ameeleza kughadhabishwa na mazingira duni yanayowazunguka watoto.

Afisa huyo alisema Jumatatu kuwa tangu kufungwa kwa shule, wameokoa watoto 52 ambao walikuwa wametoroka nyumbani na kuanza maisha barabarani.

Kauli mbiu ya mwaka huu wa 2020 ni ‘Upataji wa Mfumo wa Haki zilizo za Kirafiki kwa Watoto Barani Afrika’.

Akizungumza katika majengo ya Uhuru na Kazi mjini Mombasa, Bw Nzege alisema migogoro kati ya wazazi ndiyo sababu kuu ya watoto hao kutoroka nyumbani.

“Wanapokuwa barabarani, watoto wako katika hatari ya kunajisiwa, kulawitiwa, kushawishiwa kuingia katika utumizi wa dawa za kulevya, uhalifu, miongoni mwa balaa nyinginezo.

Mwenyekiti wa kitaifa wa watoto Rukayyah Mohammed alisema tangu kufungwa kwa shule kufuatia kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19, watoto wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali.

Miongoni mwa changamoto hizo ni kukosa sodo, kushindwa kufuatilia masomo yanayoendelezwa kupitia vyombo vya habari vya serikali kwa kukosa runinga na uwezo wa kununua vifurushi vya data.

Mtoto mwingine mmoja wa kike alisema kukosa kwa bidhaa muhimu kunawalazimu kutafuta msaada kutoka kwa wanaume ambao wanaishia kuwanajisi.

“Wengi wetu tunakosa bidhaa muhimu na hivyo tunashawishika kukubali urafiki kutoka kwa wanaume ambao watatutimizia mahitaji,”akasema.

Wazazi walihimizwa kuacha kuwatumia watoto kama vitega uchumi.

Bw Nzege alisema baadhi ya watoto wanatumiwa kuokota chupa na hata kuwa ombaomba wa mitaani.

Siku hii ni ya kukumbuka mauaji waliofanyiwa wanafunzi wa Soweto nchini Afrika Kusini Juni 16, 1976.