Makala

SIKU YA MAMA: Selina Awinja aeleza jinsi anavyowalea wanawe saba

May 11th, 2020 3 min read

Na PHYLLIS MUSASIA

WANAWAKE wengi Jumapili walisherehekea na kuthaminiwa kwa njia mbalimbali ikiwa ni Siku ya Mama.

Baadhi walituzwa zawadi kemkem na wapendwa wao.

Majukwaa ya mitandao ya kijamii kama vile Facebook yalifurika picha kadha za kina mama nchini na duniani kwa jumla nyingi zikiwa zimeambatanishwa maelezo na sifa kwa akina mama wazazi na wake wa baadhi ya watumiaji mitandao ikiwa sehemu ya kuthamini majukumu yao ya kipekee.

Hata hivyo, baadhi hawakusherekea lolote sio ati walikosa wale wa kuwatambua ila hali ngumu ya maisha inayosababishwa na janga la corona imezidi kuwabana kila kuchao.

Wakati wa mbwembwe hizo, Taifa Leo ilifanikiwa kukutana na Bi Selina Awinja wa eneo la Nairobi Area mtaani Free Area, Kaunti ya Nakuru ambapo tulisemezana naye kuhusu siku hiyo muhimu.

Bi Awinja ambaye ana watoto saba alisema hakuwa na ufahamu kwamba siku hiyo ilikuwa ya kina mama duniani ila la muhimu kwake lilikuwa kufanya bidii na kuona kwamba wanawe hawakosi chakula.

“Kuhusu siku ya kina mama duniani, nimesikia kutoka kwenu. Sikuwa na ufahamu na kufikia sasa hamna aliyenitumia ujumbe siku hii,” akasema Bi Awinja kwa tabasamu ya uoga.

Bi Awinja amekuwa mzazi wa pekee kwa wanawe kwa zaidi ya muda wa miaka minane na kulingana naye, safari nzima imekuwa ya milima na mabonde.

“Kwa zaidi ya miaka minane, sijapumzika. Nimekuwa mama na baba kwa watoto wangu. Wamenitegemea kwa chakula, mavazi, karo ya shule, matibabu na mahitaji mengine mengi na bado ninaendelea,” akaeleza.

Wakati huu wa janga la corona Bi Awinja alisema umekuwa mgumu zaidi ikilinganishwa na siku za hapo awali.

Mama huyo shujaa alikuwa akifanya kazi ya vibarua katika hoteli mbalimbali mjini Nakuru kabla ya Wizara ya Afya kutoa kanuni mpya ili kukabili maambukizi ya virusi vya corona.

Kazi hizo Bi Awinja alisema hazipo tena na amelazimika kukaa nyumbani kwa muda wa miezi miwili.

Bi Selina Awinja akiwa na baadhi ya wanawe katika mtaa wa Free Area, Nakuru Mei 10, 2020. Anawalea wanawe saba. Picha/ Cheboite Kigen

Aidha, vibarua vinginevyo alivyofanya kama vile kuosha nguo za watu katika mitaa mbalimbali vilipunguka na hata baadhi vilikatika kufutia hali ngumu; mawimbi yanayoyumbisha watu huku na kule.

“Wakati huu kupata pesa ni vigumu sana. Hata wale waliozoea kuniita niwafulie nguo mnamo wikendi hawanipigii simu tena. Nikiwatembelea nyumbani kwao hata milango hawafungui tena kwa hofu kuwa huenda wakaambukizwa virusi vya corona,” akasema.

Ukosefu wa kazi umemlazimu Bi Awinja kukata bajeti ya nyumbani hadi nusu ili kujikimu kimaisha.

Mara nyingi, familia hii imelazimika kula mara moja tu kwa siku sababu ikiwa ni changamoto za kiuchumi.

“Mara si moja tumelazimika kula githeri pekee kwa siku ili kuhifadhi pesa kidogo kwa ajili ya chakula cha siku inayofuata,’’ akaongeza.

Jambo linalompa amani Bi Awinja ni kuona kwamba angalau wanawe hawalali njaa licha ya matatizo.

Bi Awinja na wanawe wanaishi katika chumba kimoja ambapo wanalipa kodi ya Sh2,500 kila mwezi.

Ili kuendelea kusukuma gurudumu la maisha, Bi Awinja amebuni mbinu mpya ya kupata hela msimu huu wa janga la corona.

Alisema ametengeneza urafiki na wafanyibiashara katika soko la Free Area ambapo anashirikiana nao na kuwasaidia kuuza bidhaa mbalimbali.

“Wengi wao wananijua na kufahamu hali yangu. Ninaweza nikapata kazi ya kuuza bidhaa sokoni kwa muda wa kati ya saa nne na tano kisha kulipwa Sh200,” akasema.

Licha ya kwamba Sh200 haziwezi kutosha mahitaji ya familia yake, Bi Awinja alisema ni heri kuliko kukosa.

Yeye hushirikiana na mwanawe wa kike aliyekamilisha elimu ya kidato cha nne mwaka 2019 ili kukimu baadhi ya majukumu.

“Baada ya mwanangu kifungua mimba kukamilisha elimu ya sekondari na kupata alama ya B+ amekuwa wa msaada mkubwa sana kwangu na familia kwa jumla. Anafahamu hali ilivyo na amejitolea kunisaidia,” akasema Bi Awinja aliyeongeza kuwa msichana huyo anasubiri kujiunga na chuo kikuu.

Alifichua kwamba, aliwahi kuwa mke na kuishi maisha bora kama wanawake wengine lakini matatizo ya ndoa kama vile ukosefu wa uaminifu ulisababisha ndoa hiyo kuvunjika.

Hata hivyo, baba ya watoto wake hajaweza kuajibika tena tangu wakati huo.

Alisema familia yake haijaweza kufaidika na vyakula vya misaada vinavyotolewa na serikali ya kaunti licha ya chifu wa eneo hilo kuchukua orodha wiki tatu zilizopita.

“Niliandikisha familia yangu kwa orodha ya familia ambazo zilinuia kufaidika na msaada wa vyakula vya dharura chini ya serikali ya kaunti lakini kufikia sasa sijapata lolote,” akasema.

Bi Awinja anatumai kuwa janga hili la corona litapita hivi karibu na hali ya kawaida kurejea nchini.

Aliwataka kina mama wanaolea watoto bila baba zao kujikakamua na kumtumainia mwenyezi Mungu kwa kila jambo.

“Tunaishi katika nyakati tofauti lakini tusififie katika kufanya bidii kwa ajili ya watoto wetu. Tuwe imara na kumtumainia Mungu wakati wote,” akasema Bi Awinja na kuwatakia kina mama wote siku njema ya kina mama duniani na yenye baraka.