Habari za Kitaifa

Siku ya kufa kupona kwa Maribe na Jowie katika kesi ya mauaji

February 9th, 2024 1 min read

NA SAM KIPLAGAT

HUKUMU dhidi ya mwanahabari wa zamani wa runinga Jacque Maribe na mchumba wake wa zamani Joseph Irungu, ‘Jowie’, inatolewa Ijumaa, Februari 9, 2024 baada ya kuahirishwa mara tatu awali.

Jaji ya Mahakama Kuu Grace Nzioka alisogeza karibu tarehe ya hukumu hiyo, baada ya kutangaza mwezi jana kwamba itatolewa Machi 15.

Jaji huyo aliiahirisha Januari 26 baada ya Maribe kukosa kufika mahakamani kwa madai kwamba anaugua.

Kuahirishwa huko kulikuwa kwa tatu mfululizo baada ya kuahirishwa Oktoba 6 na Desemba 15 mwaka jana.

Bi Maribe na Bw Irungu wameshtakiwa kwa mauaji ya mfanyabiashara Monicah Kimani, kosa ambalo linadaiwa kufanyika usiku wa Septemba 19, 2018.

Mfanyabiashara huyo aliyekuwa na umri wa miaka 28 alikuwa amewasili nchini kutoka Sudan Kusini, na kwenda kwa makazi yake ya Lamuria Garden.

Upande wa mashtaka uliambia mahakama kwamba mwanamke huyo aliwasili katika uwanja wa JKIA saa kumi na mbili jioni, akitokea Juba ambako alikuwa anafanya biashara za kifamilia. Alimpigia simu kakake, George Kimani, kumwambia kuwasili kwake.

Alichukuliwa uwanja wa ndege na Bw John Otieno, mwanateksi na kumfikisha kwake Lamuria Garden, halafu yeye akaenda zake.