HabariMakala

SIKU YA WANAWAKE DUNIANI: Mama mjane mchoraji

March 8th, 2019 3 min read

Na GEOFFREY ANENE

HUKU ulimwengu mzima ukiadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2019 mnamo Machi 8, mama Cecilia Nambuye Simiyu, ambaye ni mchoraji hodari, ameomba wahisani kumsaidia kukamilisha masomo yake ya Shule ya Upili.

Taifa Leo ilikutana na mama huyu wa watoto watano katika makutano ya barabara za Ronald Ngala na Tom Mboya mnamo Machi 2 na tena Machi 8 katika makutano ya barabara ya Race Course Road na River Road karibu na eneo la OTC.

Mama Cecilia Nambuye Simiyu akichora picha ya mtawa Mama Teresa mnamo Machi 2, 2019. Picha/ Geoffrey Anene

Aligusa wakazi wa jiji la Nairobi na talanta yake ya hali ya juu ya uchoraji.

Licha ya kuwa hakuwa tayari kutusimulia maisha yake, anasema anachohitaji zaidi ni kusaidiwa na wala si kuonekana katika vyombo vya habari.

“Kuonekana katika vyombo vya habari hakuweki chakula mezani. Niliwahi kutembelea shirika moja la habari na nikahojiwa kwenye runinga nikiahidiwa nitapokea usaidizi, lakini halikutimiza ahadi yake. Pole, mwanangu siwezi kukuhadithia maisha yangu isipokuwa tu kwamba katika familia yetu, tulizaliwa watoto wawili – mimi na ndugu yangu ambaye yuko nyumbani katika eneo bunge la Turbo katika kaunti ya Uasin Gishu. Babangu aliaga dunia nikiwa na umri wa miaka sita. Ningependa kuendeleza masomo yangu na kujiendeleza kimaisha. Mimi huzunguka jijini Nairobi nikifanya kazi hii ya uchoraji. Mimi huzima simu kutoka ninapofika jijini ili niweze kumakinikia kazi yangu. Naifungua jioni,” anasema Simiyu, ambaye yuko katika kidato cha tatu katika shule moja jijini Nairobi.

Wakati wa mahojiano haya mafupi, Bi Simiyu alilalamika hana mahali maalumu pa kufanyia kazi.

Mama Cecilia Nambuye Simiyu akichora. Picha/ Geoffrey Anene

Shughuli yake hutatizwa na wafanyabiashara wengi anapotafuta mahali pa kukaa ili achore.

Katika siku ya kwanza, alikuwa ameketi hatua chache kutoka duka moja kuchora, huku akiwa na boksi ya kuombea fedha.

Watu walimiminika katika eneo alilokuwa ameketi. Wengi hawakuamini macho yao kwamba mama huyo, ambaye alifanya mtihani wake wa darasa la nane mwaka 2010, ni mchoraji hodari.

“Hii ni changamoto kubwa sana kwa vijana,” bwana mmoja aliyevutiwa na kazi ya Simiyu alisikika akisema, huku wapitanjia wengi wakisifu kazi ya mama huyo na kutumbukiza sarafu za Sh1, Sh5, Sh10, Sh20 na pia noti hasa za Sh50 na Sh100 katika boksi hilo.

Mahali hapo tu, kulikuwa na jamaa wawili walioonekana kukerwa zaidi na kuwepo kwa mama huyo hapo.

“Mama hizo fedha umekusanya zimetosha, hebu toka hapa. Unaweza kunichora, hebu chora fulani,” mwanamume mmoja kati ya jamaa hao wawili wasumbufu alisikika akisema na kupitapita katikati ya watu na nyuma na mbele ya mama huyo.

Katika bango moja analotembea nalo, mama huyo ameandika kwa wino akisema yeye ni mjane na mtu aliyewahi kuwa bila makao.

Bango hilo linasema kwamba aliokolewa kutoka barabara za Nairobi na kupelekwa katika kituo cha kupata ushauri na kurekebisha tabia cha Kariokor katika eneobunge la Starehe kwa miaka miwili.

Baadhi ya picha alizochora Mama Cecilia Nambuye. Picha/ Geoffrey Anene

Alihamishiwa katika kituo kingine cha kurekebisha tabia cha Kayole katika eneo bunge la Embakasi Central kwa miaka mitatu.

“Baada ya kukamilisha vipindi hivyo vya kurekebishwa tabia, mimi nimebadilika. Niliamua kurejea shuleni. Nilifanya mtihani wangu wa Shule ya Msingi (KCPE) mwaka 2010 na sasa niko katika kidato cha tatu. Tafadhali nisaidie nipate vifaa vya masomo,” bango hilo linasema katika lugha ya Kiingereza.

Vifaa vyake vya uchoraji ni shashi, rula, kalamu ya kawaida, penseli ya rangi, raba na mashine ya kuchonga kalamu (sharpener). Pia, anatembea na shubaka la mbao la kuwekea picha alizochora. Mama huyu amechora watu mashuhuri.

Wapita njia wastaajabishwa na talanta ya Mama Cecilia Nambuye Simiyu katika uchoraji. Picha/ Geoffrey Anene

Katika picha moja, amechora Rais Uhuru Kenyatta akisalimiana na kinara wa Nasa Raila Odinga shughuli ambayo kwa kimombo inafahamika kama ‘handsheki’.

Pia, kuna picha ya Jaji Mkuu David Maraga, Inspekta Generali wa Polisi Joseph Boinet na Magavana Mike Sonko (Nairobi) na Jackson Mandago (Uasin Gishu), na wakili Miguna Miguna, miongoni mwa picha zingine.

Zote zimetiwa kwenye fremu. Katika shubaka lake pia kuna stakabadhi yake ya kuonyesha alikamilisha Shule ya Msingi na pia kitambulisho chake cha kitaifa.

Tulipokutana mara ya kwanza, mama huyo, ambaye alikuwa amevalia nguo ndefu nyekundu, sweta ya kijani kibichi na slipa, alionyesha weledi wake wa kuchora alipoanza kuchora mtawa Mama Teresa na kuikamilisha baada ya dakika chache.