Habari Mseto

SIKU YA WAZEE DUNIANI: Wakongwe wanastahili malezi mema

October 2nd, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKONGWE wanastahili kupewa malezi bora ili waweze kuboresha hali yao ya maisha.

Mkurugenzi wa Ahadi Kenya Dkt Stanley Kamau alisema Jumanne uchunguzi uliofanywa umebainisha kuwa wazee wengi katika vijiji wamedhalilishwa na kuachwa pweke bila yeyote wa kuwalinda.

“Kutokana na hali hiyo, ni vyema serikali kuu na za kaunti zishirikiane na ili kuona ya kwamba wakongwe hao wanajengewa vituo vitakavyowasaidia kwa kujali afya zao,” alisema Bw Kamau.

Mkurugenzi wa Shirika la Ahadi Kenya Dkt Stanley Kamau (kulia) akihutubia waandishi wa habari Oktoba 1, 2019, eneo la Gatundu Kusini. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema wazee hao wakijumuika pamoja wanapata mwamko mpya katika nafsi zao na bado wanaweza kuishi muda mrefu bila shida nyingi.

Aliyasema hayo mnamo Jumanne wakati wa kuadhimisha Siku ya Wazee Duniani katika Kanisa Katoliki la Wamwangi eneo la Gatundu Kusini ambapo wazee wapatao 500 walihudhuria hafla hiyo.

Alisema serikali ilipofanya sensa ya hivi majuzi iliweza kupata idadi kamili ya wakongwe kote nchini na kwa hivyo inaweza kufanya mipango bora kuhusu matakwa yao.

Kutembelea wazazi

Alitoa mwito kwa watu wote walio na wazazi wao vijijini wawe wakifanya juhudi kuona ya kwamba wanawatembelea kila mara ili kuwaliwaza.

“Hakuna haja ya kuishi mjini kwa muda mrefu bila kufanya juhudi ya kuwatembelea wazazi vijijini. Iwapo tutawajali bila shaka hata tutapata baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu,” alisema Bw Kamau.

Bi Regina Wanderi ambaye ni mwalimu wa kutoa ushauri kwa umma alisema wazee wengi katika vijiji wamekosa watu wa kuwahudumia huku wengi wakikosa hata chakula.

“Wengi wao wanahitaji viti vya magurudumu, na hata mikongojo ya kutembelea. Wazee hao wakiachwa peke yao hubaki pweke huku wakishindwa kujitegemea,” alisema Bi Wanderi.

Bi Joyce Wanjiku Ngugi, mwenyekiti wa maswala ya watoto, alisema wakongwe hao mara nyingi huachwa na watoto wadogo kuwalea huku mabinti zao wakipotelea mijini kwa shughuli zingine.

“Ni vyema pia wakongwe wakipata nafasi ya kujituliza bila kusumbuliwa na mambo mengi yenye kuleta msongo wa mawazo. Mtu akifikisha umri wa miaka 70 anastahili kutuliza akili na kutafakari mambo yake mwenyewe,” alisema Bi Ngugi.