HabariSiasa

Sikujua mkataba niliotia saini utageuzwa, sasa nitauvunja – Sonko

April 23rd, 2020 2 min read

BENSON MATHEKA Na COLLINS OMULO

GAVANA wa Kaunti ya Nairobi, Bw Mike Sonko sasa anatishia kuvunja mkataba wa kuhamisha majukumu muhimu katika kaunti hiyo hadi serikali ya kitaifa akidai alidanganywa na maafisa wa serikali.

Haya yanajiri baada ya juhudi za kutaka kunyakua majukumu aliyokabidhi serikali ya kitaifa kugonga mwamba huku shirika la huduma ya jiji la Nairobi (NMS) likimlaumu kwa kulihujumu.

Bw Sonko anasema ameanza harakati za kuvunja mkataba wa kuhamisha majukumu hayo akisema pia anahujumiwa na kudharauliwa.

Kulingana na Sonko, ingawa yeye na Rais Uhuru Kenyatta walikuwa na nia njema, baadhi ya maafisa serikalini wanampiga vita.

“Nimeanza mchakato wa kuutamatisha mkataba wa kuhamisha majukumu kama mkataba wa kawaida unavyovunjwa. Binafsi nitaenda kortini kuomba uvunjwe,” alisema.

Bw Sonko alikiri kwamba hakupewa muda wa kusoma mkataba huo aliotia sahihi katika Ikulu ya Nairobi mnamo Februari 25 mwaka huu na kufikia sasa, hajakabidhiwa nakala.

“Niliambiwa kilikuwa kitu kizuri kuhudumia wakazi wa Nairobi nikiendelea na kesi yangu kortini. Nilikubali bila kusoma stakabadhi yenyewe. Sikujua itatugeuka,” alisema.

Hata hivyo, kulingana na mkataba huo, unaweza kutamatishwa pande zote zikikubaliana kupitia maandishi na baada ya kushindwa kusuluhisha tofauti zikiibuka.

Mnamo Jumanne, Bw Sonko alilaani maafisa wakuu serikalini kwa kutumia polisi kubomoa vibanda alivyoweka katika maeneo tofauti jijini kunyunyizia watu dawa kuzuia maambukizi ya corona.

“Naomba wale waliotusimamisha kunyunyizia dawa mitaa ya jiji na ya mabanda, kugawa chakula, maski na sanitaiza wachomeke jehanamu,” Sonko aliandika katika kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Alisema vibanda hivyo alivyoweka katika kituo cha mabasi cha Kencom katikati ya jiji, katika ofisi ya naibu kamishna wa Kibra, na mtaani Buruburu ni sawa na ambavyo Gavana Hassan Joho aliweka katika Kaunti ya Mombasa.

Kuvunjwa kwa vibanda hivyo kulijiri siku chache baada ya serikali kupiga marufuku kundi lake la Sonko Rescue Team kugawa chakula kwa wakazi wa mitaa ya mabanda jijini Nairobi na kunyunyizia dawa mitaa hiyo.

Vilevile, ilijiri wiki moja baada ya juhudi zake za kupinga hatua ya serikali kuhamisha wafanyakazi wa Kaunti ya Nairobi hadi NMS akidai hatua hiyo haikuwa ya kisheria.

Mkurugenzi Mkuu wa NMS Muhammad Badi alimlaumu kwa kuhujumu shirika hilo licha ya kutia sahihi mkataba wa kuhamisha majukumu muhimu ikiwemo idara ya afya kwa serikali ya kitaifa.

Bw Sonko anadai kuwa watu wenye ushawishi serikalini waliokuwa wakimpiga vita asiangamize mitandao ya ufisadi katika serikali ya Kaunti ya Nairobi, wameungana kumzuia asisaidie wakazi wa Nairobi wakati huu wa kupigana na janga la corona.

Gavana huyo anakabiliwa na kesi ya ufisadi na amezuiwa kukanyaga ofisini mwake.Kulingana naye, Sonko Rescue Team ni shirika lisilo la kiserikali lililosajiliwa sawa na wakfu wa Joho katika Kaunti ya Mombasa na kumzuia kusaidia wakazi wa Nairobi ni kumpiga vita.

Alidai ni katibu wa wizara ya usalama wa ndani, Dkt Karanja Kibicho na mshirikishi wa eneo la Nairobi Wilson Njega walioagiza vibanda hivyo kubomolewa.Bw Sonko aliwahakikishia wakazi wa Nairobi kwamba hatachoka kuwasaidia.

“Watu wangu, hata iweje, sitavunjika moyo. Huu sio wakati wa siasa duni bali Ni wakati wa kuungana na kufanya kila tuwezalo kuzuia kusambaa kwa janga la corona ikiwa ni pamoja na kufanya umma unaotaka usaidiwe ili kuwa salama,” alisema Bw Sonko.

Afisa mmoja wa utawala eneo la Kibra aliyeomba tusitaje jina alisema vibanda hivyo vilibomolewa ili kumpa funzo Bw Sonko kwa kupiga vita NMS.

“Hauwezi kushindana na serikali, ina njia nyingi za kukuzima. Kuna hisia kwamba Sonko anatumia kundi lake kuteka majukumu aliyokabidhi serikali ya kitaifa ambayo yanasimamiwa na NMS,” alisema afisa huyo na kuongeza kuwa michango ya kusaidia vita dhidi ya corona inafaa kupitishiwa kamati ya kukabiliana na janga hilo.