Habari Mseto

Sikujua nguo nilizouziwa ni sare za kijeshi, muuzaji mitumba ajitetea kortini

November 10th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MUUZAJI nguo kuu kuu almaarufu mitumba alishtakiwa Jumanne kwa kupatikana na sare za kijeshi. Samuel Waithaka Kamau alifikishwa mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya Milimani Bi Jane Kamau na kukanusha shtaka dhidi yake.

Bw Kamau alikabiliwa na shtaka kwamba mnamo Novemba 6, 2020 katikati ya jiji la Nairobi alipatikana na magwanda ya kijeshi, jaketi 77, suruali ndefu za kijeshi 64.

Mahakama ilielezwa na kiongozi wa mashtaka Bw Fredrick Kimathi kwamba mshtakiwa alijua magwanda hayo yalipatikana kwa njia isiyo halali ama zimeibwa.

Lakini mshtakiwa ambaye hakuwa amewakilishwa alijitetea na kueleza korti kwamba alinunua robota Gikomba na alipoifungua alipata ni magwanda ya kijeshi.

“Naomba mheshimiwa uniachilie kwa dhamana kwa vile mimi nauza nguo kuu kuu kati kati ya jiji. Nilinunua robota la nguo hizi kutoka Gikomba na nilipoifungua nikapata ni nguo za kijeshi,” alifichua Waithaka.

Mshtakiwa aliendelea kumweleza hakimu,” Nilipogua robota liko na nguo za kijeshi nilienda kwa afisa mkuu wa polisi kituo cha polisi cha Central nikamweleza lakini akanieleza atatuma maafisa kuziangalia.Nilikamatwa na kushtakiwa.”

Aliomba korti imwonee huruma na kumwachiliwa kwa dhamana na pia kuamuru nguo hizo zitwaliwe na idara husika.

Lakini kiongozi wa mashtaka Bw Kimathi aliomba korti impe mshtakiwa muda awasilishe kortini risiti alikonunua robota hilo ndipo aishauri mahakama jinsi ya kufanya na nguo hizo.

Hata hivyo aliomba korti imwachilie mshtakiwa kwa dhamana. Mahakama iliwaachilia kwa dhamana yaa Sh100,000 pesa tasilimu.