NA RICHARD MUNGUTI
WAKILI Paul Ndung’u aliyeongoza jopo kuhusu umiliki wa mashamba, Jumatatu aliambia Mahakama Kuu kuwa hajui iwapo hayati Daniel arap Moi alilipwa Sh10 milioni za shamba ambalo umiliki wake una mzozo.
Bw Ndung’u aliyekuwa anatoa ushahidi katika kesi ya mzozo wa umiliki wa shamba hilo lenye thamani zaidi ya Sh500 milioni, alisema alitayarisha cheti cha mauzo ya shamba hilo na kumpelekea hayati Moi katika Ikulu ya Nairobi akiandamana na aliyekuwa waziri wa Fedha marehemu Arthur Magugu.
“Ulishuhudia hayati Moi akitia saini cheti cha kuuza shamba hilo?” wakili Julius Kemboi anayewakilisha familia ya Moi alimuuliza Ndung’u.
Bw Ndung’u alimweleza Jaji Samson Okong’o kwamba hakushuhudia Moi akitia saini cheti cha kuuza shamba hilo.
“Tulienda Ikulu ambapo marehemu Magugu alimweleza sababu yetu kuenda kisha akampa cheti cha kuuza akitie saini,” Bw Ndung’u alijibu.
Mahakama ilielezwa kuwa shamba hilo liliuziwa kampuni ya DPS International Limited anayoimiliki.Umiliki wa shamba hilo unazozaniwa na USIU, Kampuni ya mmiliki wa Benki ya Equity James Mwangi na George Kiongera ijulikanayo Maestro Connections Health System Ltd.
Ndung’u alieleza mahakama kuwa Bw Moi na mkewe Magugu aliuzia kampuni yake ijulikanayo DPS International kwa bei ya Sh10m.
Alieleza kwamba cheti cha mauzo ya shamba hilo kilisalia katika kampuni ya mawakili ya H H Mathews alipoondoka lakini hatimaye akaombwa na USIU afike kortini kutoa ushahidi.
USIU inadai ilinunua shamba hilo kutoka kwa kampuni ya bima ya Insurance Company East Africa kwa bei ya Sh90 milioni 1999.
Subscribe our newsletter to stay updated