Michezo

Silibwet, Busia Wolves na Egerton zavuna pointi tatu

March 13th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Silibwet FC na Busia Wolves kila moja iliachia pointi tatu muhimu kwenye mechi za Kundi B Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza msimu huu.

Nao wachana nyavu wa Transfoc FC walijikuta kwenye wakati mgumu walipokubali kupokezwa kipigo cha bao 1-0 na Egerton FC kwenye mechi iliyochezewa uwanjani Kericho Stadium mjini humo.

Hatua ya Transfoc kuyeyusha mchezo wa pili pili mfululizo ilifanya maofisa wake kukwepa kuzungumza na wanahabari wa michezo kwa kuzingatia ilipigiwa chapuo ingelipiza kisasi ilipozaba mabao 3-0 na Zoo Youth.

Bungoma Superstars na GFE 105 kila moja ilituzwa alama tatu bila jasho ushindi wa mezani baada ya wapinzani wao Silibwet na Busia Wolves mtawalia kusepa.

Baada ya Peter Joma na Joseph Hangida kucheka na nyavu mara moja kila mmoja waliibeba Zoo Youth kuponda Maafande wa APs Bomet mabao 2-0 na kuibandua kileleni Vihiga Bullets iliyovuna mabao 2-0 mbele ya Transmara Sugar FC.

”Hakika tunaweza ila tunahitaji kujitahidi zaidi ili kufanya kweli na kunasa tiketi ya kusonga mbele msimu ujao,” Peter Anyona mchezaji wa Zoo Youth alisema. Matokeo hayo yaliifanya Zoo Youth kutwaa usukani kwa alama 21 sawa na Bungoma Superstars.

Kwenye mechi hizo, Bondo United iliichoma Muhoroni Youth bao 1-0 lililofumwa na Kevin ‘Dimore’ Omondi, nao Ben Wagema na Reuben Okoth kila mmoja alipiga moja safi na kubeba St Josephs Youth Academy kukomoa Raiply FC mabao 2-0 huku Kisumu Allstars ikitia kapuni magoli 4-0 mbele ya Poror Mote.