Habari Mseto

Simanzi yamzidia Kori mkewe Mary Wambui akizikwa kifahari

March 3rd, 2019 1 min read

Na Nicholas Komu

MAJONZI yalimzidi Joseph Kori jana katika mazishi ya mkewe Mary Wambui mjini Mweiga, Kaunti ya Nyeri, akalazimika kumpisha rafiki asome ujumbe wa rambirambi aliomwandikia marehemu mkewe.

Hata wavulana wao wawili walipotoa rambirambi zao Bw Kori hakutamka lolote kwenye ibada hiyo ya mazishi iliyofanyika katika uwanja wa ndege wa Shirika la Wanyamapori (KWS) wa Mweiga.

Marehemu Wambui alipewa heshima ya hadhi ya juu huku jeneza lake likibebwa kwa gari la kifahari la Mercedes.

Maelfu ya waombolezaji walihudhuria mazishi hayo huku wakimtaja Wambui kama mtu mchangamfu na mwenye furaha.

Wakiwa wamevalia suti za buluu, Bw Kori aliketi kando ya wanawe wawili Derrick Kamangara na Hayden Karue huku akitiririkwa na machozi mara kwa mara.

Katika ujumbe wake uliosomwa na rafiki, Bw Kori alimtaja mkewe kama mtu mchangamfu na wakati wote alikuwa tayari kumsaidia mtu yeyote aliyekuwa na shida.