Michezo

'Simba wa Nairobi' wanguruma

February 3rd, 2020 1 min read

NA JOHN KIMWERE 

WAPIGAGOZI wa Nairobi City Stars maarufu Simba wa Nairobi walitoka chini goli 1-0 na kufaulu kubeba mabao 2-1 dhidi ya Bidco United, kwenye patashika ya kuwania taji la Betika Supa Ligi ya Taifa (BNSL) iliyopigiwa Hope Center Kawangware, Nairobi.

Bidco ilipokezwa kichapo hicho licha ya kocha wake, Anthony Akhulia kujipiga kifua kwamba wangezima wapinzani wao kwenye patashika hiyo.

Kocha huyo siku moja kabla ya mchezo huo alinukuliwa akisema ”Kiukweli hatuna la ziada bali tumepania kujitahidi kiume kuhakikisha tutashinda City Stars ili kuipiga breki kwenye kampeni zake.”

City Stars ya kocha, Sanjin Alagin ilijiongezea ushindi wa alama tatu pale, Anthony Kimani na Jimmy Bageya walipotikisa wavu mara moja kila mmoja. City Stars imeweka pengo la pointi kumi dhidi ya Bidco United ambapo inaongoza kwa alama 55.

Nao Douglas Mokaya na Patrick Mugendi kila mmoja alipiga kombora moja safi na kusaidia Nairobi Stima kunyanyua Ushuru FC mabao 2-0 na kuendelea kushikilia tatu bora kwa alama 42, tatu mbele ya Vihiga United iliyozoa ushindi wa mezani dhidi ya Murang’a Seal.

Nazo Vihiga Bullets na FC Talanta zilikubali kulala kwa mabao 2-0 na mabao 5-0 mbele ya Modern Coast Rangers na Coast Stima mtawalia.

Samuel Ate na Collins Adimu walitupia kambani mabao ya Modern Coast huku Erick Ombija akifungia Coast Stima mabao mawili. Magoli mengine yalipatikana kupitia Rodgers Okumu, Dominic Waithaka na Abdul Khamis waliojaza moja kila mmoja.

Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, wachana nyavu wa kikosi cha Shabana FC walilazimisha kutoshana nguvu mabao 2-2 na St Josephs Youth, Maafande wa APs Bomet walitoka bao 1-1 na Fortune Sacco, Administration Police iliagana sare tasa na Kibera Black Stars nayo Mt Kenya United ilipondwa mabao 4-0 na Kenya Police.