Michezo

Simbas yajiandaa kwa Victoria Cup Floodlit ikiwadia

September 12th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Kenya cha raga ya wachezaji 15 kila upande almaarufu Simbas kitaanza mazoezi mwishoni mwa wiki hii chini ya mkufunzi Paul Odera kwa minajili ya kivumbi cha Victoria Cup mnamo Septemba 21.

Kipute hicho kitakachoandaliwa mjini Nakuru, kiwakutanisha Simbas na Sables wa Zimbabwe waliopepeta Kenya 30-29 katika mchuano wa mkondo wa kwanza mnamo Agosti jijini Bulawayo.

Odera amefichua uwezekano wa kuwawajibisha wanaraga wazoefu zaidi dhidi ya Zimbabwe licha ya chipukizi aliowategemea wiki mbili zilizopita kubwaga Zambia 31-16 uwanjani RFUEA, Nairobi.

“Huu ndio mchuano wetu mkubwa zaidi na wa mwisho kabisa mwaka huu. Hivyo, tunalenga kukamilisha kampeni za msimu kwa matao ya juu zaidi,” akasema Odera.

Kukamilika kwa mapambano ya Victoria Cup kutawapa wanaraga wa Simbas kurejea katika vikosi vyao ili kujiandaa kwa kipute cha Impala Floodlight ambacho kimeratibiwa kupigwa kati ya Septemba 28 na Oktoba 12, 2019.

Mwenyekiti wa Impala, Bob Asiyo amesema mialiko tayari imetolewa kwa klabu mbalimbali kufanikisha kampeni hizo za Floodlight huku droo ikitarajiwa kufanywa wiki ijayo.

Wanabenki wa KCB ambao pia ni wafalme wa Raga ya Kitaifa ya 7’s ndio mabingwa watetezi wa kivumbi hicho.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Raga la Kenya (KRU), kiini cha kuandaliwa kwa Victoria Cup mjini Nakuru ni kutoa burudani kwa mashabiki wa mchezo huo mashinani na kuwapa wanaraga chipukizi jukwaa mwafaka zaidi la kuchochea vipaji vyao.

Itakuwa mara ya pili mwaka huu kwa mchuano wa haiba kubwa katika ulingo wa raga kuchezewa nje ya jiji la Nairobi baada ya Kisumu kuwa mwenyeji wa mkondo wa kwanza wa kivumbi cha Elgon Cup kati ya Kenya na Uganda mnamo Juni.

Zimbabwe wanaoongoza jedwali kwa alama 17, watashuka ugani kwa minajili ya mchuano huo wakitarajia kuendeleza rekodi nzuri ya kutopigwa katika Victoria Cup hadi kufikia sasa msimu huu. Kenya inashikilia nafasi ya pili kwa pointi 16.

Zimbabwe watakuwa wenyeji wa Zambia wikendi hii, na huenda wakatawazwa mabingwa wa Victoria Cup iwapo watasajili ushindi dhidi ya majirani zao hao.

Kushika mkia

Uganda ambayo tayari imekamilisha kampeni zake zote katika kipute cha Victoria Cup inashikilia nafasi ya tatu kwa alama 15 huku Zambia ikikokota nanga mkiani bila alama yoyote baada ya kushindwa kusajili ushindi au sare yoyote kufikia sasa.

Kenya itashuka dimbani wiki mbili baada ya kuteremka chini kwa nafasi moja zaidi hadi nambari 34 kwenye orodha ya viwango bora vya raga ya Shirikisho la Raga Duniani. Zimbabwe waliokuwa katika nafasi ya 32 duniani kwa sasa wameshuka hadi nafasi ya 33.

Zimbabwe ambao walipepeta Uganda 32-26 jijini Harare katika mechi ya nne ya Victoria Cup kwa sasa ni ya tatu katika viwango bora vya Afrika baada ya Afrika Kusini na Namibia zinazoshikilia nafasi za tano na 23 duniani mtawalia. Zimbabwe wanajivunia alama 51.74 kutokana na ufanisi wa kucharaza Uganda 32-26 katika mechi ya marudiano ya Victoria Cup. Ushindi wa Uganda dhidi ya Zambia katika mchuano uliopita umewapaisha hadi nafasi ya 41.