Michezo

Simbas hatimaye wapata kocha mpya

March 20th, 2018 1 min read

Kocha mpya wa Simbas Ian Snook kutoka New Zealand. Picha/ Hisani

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji 15 kila upande almaarufu Simbas hatimaye imepata kocha mpya Ian Snook kutoka New Zealand, wiki 15 baada ya kutengana na raia wa Afrika Kusini Jerome Paarwater.

Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) lilitangaza Machi 19 kwamba Snook amekubali kuinoa Simbas kama kocha mkuu na kuongeza kwamba atawasili nchini wiki ya kwanza ya mwezi ujao wa Aprili.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, KRU imemsifu Snook ikisema “Analeta ujuzi wa miaka mingi kikosini baada ya kufanya kazi ya ukufunzi na kupeana ushauri nchini New Zealand, Australia, Uingereza, Jamhuri ya Ireland, Laos, Japan, Croatia, Italia na Afrika Kusini.”

Snook, ambaye amekuwa kocha kwa zaidi ya miaka 30, atasaidiwa na raia mwenzake wa New Zealand Murray Roulston, ambaye pia amefanya kazi ya kocha na kutoa ushauri kwa timu ya Highlanders na mataifa ya New Zealand, Japan, Trinidad & Tobago na Romania.

“Wawili hawa wakati huu wanashirikiana na benchi la kiufundi la Kenya linalojumuisha Dominique Habimana, Charles Ngovi, Richard Ochieng, Chris Makachia na Simiyu Wangila kuunda ratiba ya mazoezi. Watawasili mapema Aprili,” KRU ilitangaza.

Shughuli ya kutafuta mrithi wa Paarwater imekuwa ikiendelea kwa muda na hata kuzua wasiwasi kikosini baada ya kuonekana kuchukua muda mrefu sana.

Wakati huo huo, KRU imefichua kwamba inalenga kutafutia Simbas mechi kadhaa za kujipima nguvu dhidi ya timu kutoka Bara Ulaya kabla ya Kombe la Afrika la mwaka 2018 litakalotumika kuchagua mwakilishi wa Afrika katika Kombe la Dunia mwaka 2019.

Ratiba ya Simbas ya Kombe la Afrika (2018):

Juni 23 – Kenya vs. Morocco (ugenini)

Juni 30 – Kenya vs. Zimbabwe (nyumbani)

Julai 7 – Kenya vs. Uganda (nyumbani)

Agosti 11 – Kenya vs. Tunisia (nyumbani)

Agosti 18 – Kenya vs. Namibia (ugenini)