Michezo

Simbas na Lionesses walipua wapinzani wao Uganda na kuhifadhi ubingwa wa Elgon Cup

July 13th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imehifadhi mataji ya wanaume ya wanawake ya raga ya wachezaji 15 kila upande ya Elgon Cup baada ya Simbas na Lionesses kurarua Uganda kwa alama 16-5 na 33-5 mtawalia jijini Kampala, Jumamosi.

Lionesses ya kocha Felix Oloo ilikuwa ya kwanza kutawazwa malkia ilipokamilisha kampeni safi iliyoanza na ushindi wa 42-13 mjini Kisumu mnamo Juni 22 na kukamilika kwa jumla ya alama 77-18 Julai 13.

Katika mechi ya marudiano Jumamosi, Grace Adhiambo alichangia penalti mbili na mkwaju, nahodha Philadelphia Olando akapachika miguso miwili nao Stella Wafula, Leah Wambui na Janet Okello wakafunga mguso mmoja kila mmoja.

Simbas, ambayo ilikuwa chini ya kocha Albertus Van Buuren baada ya Paul Odera kusafiri nchini Brazil kwa Raga ya Dunia na timu ya Under-20 (Chipu), ilikuwa na kazi ngumu uwanjani Kyadondo.

Iliingia mechi hii ikiuguza kichapo cha alama 16-13 mjini Kisumu hapo Juni 22. Simbas ilianza vibaya mechi ya marudiano pale iliruhusu Uganda kuongoza 5-0 kupitia mguso bila mkwaju kutoka kwa Ronald Kanyanya. Nyota wa Kabras Sugar RFC Philip Wokorach alipoteza mkwaju.

Hata hivyo, Billy Omondi alisawazishia Kenya 5-5 kupitia pia mguso ambao Jacob Ojee hakufanikiwa kutinga mkwaju wake. Madhambi kutoka kwa Waganda yalimpa Ojee nafasi ya kuandikisha jina lake kwenye orodha ya wafungaji alipopachika penalti kwa ustadi na kuweka Kenya mbele 8-5.

Kenya haikulegeza kamba katika kipindi cha pili pale ilifungua mwanya hadi 11-5 kupitia penalti nyingine kutoka kwa Ojee ambaye alikamilisha ufufuo wa Simbas kupitia mguso baada ya kutimka mita 70 kutoka nusu ya Kenya alipopokea pasi murwa kutoka kwa Michael Wanjala.

Kenya yapata alama za kutosha

Ingawa Ojee hakufaulu kuongeza mkwaju wa mguso huu, Kenya ilikuwa imepata alama za kutosha kutawazwa wafalme kwa mwaka wa nne mfululizo baada ya kunyakua mataji ya mwaka 2016, 2017 na 2018 bila kupoteza mechi.

Uganda, ambayo mara ya mwisho ilishinda Elgon Cup ni mwaka 2015, iliingia mechi ya marudiano ikiamini itarejesha taji. Hata habari kutoka Uganda zilisema kuwa Cranes ilikuwa imejiandaa kusherehekea taji kwa kuwapa mashabiki kreti 50 za bia ya aina ya Nile Special bila malipo.