Michezo

Simbas washuka viwango vya raga duniani

April 30th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA Simbas imetupwa nje ya mataifa 30-bora kwenye viwango bora vya raga ya wachezaji 15 kila upande duniani Jumatatu.

Katika viwango vipya vilivyotangazwa na Shirikisho la Raga duniani (World Rugby), Kenya imeteremka nafasi moja na sasa inashikilia nambari 31 kwa alama 54.24.

Imerukwa na Korea Kusini, ambayo ilititiga wenyeji wa Kombe la Bara Asia Malaysia 35-10 jijini Kuala Lumpur hapo Aprili 28, 2018 na kupaa nafasi moja.

Kenya inasalia katika nafasi ya tatu barani Afrika nyuma ya Afrika Kusini, ambayo imesalia nambari sita duniani nayo Namibia imekwamilia nafasi ya 24 duniani.

Uganda ni ya nne barani Afrika na 34 duniani. Morocco, Tunisia na Zimbabwe zinafuatana katika nafasi za tano, sita na saba barani Afrika, mtawalia. Zinashikilia nafasi za 38, 43 na 44, duniani, mtawalia.

Kenya, Namibia, Morocco, Tunisia, Uganda na Zimbabwe zitawania taji la Kombe la Afrika la Dhahabu kati ya Juni 16 na Agosti 18 mwaka 2018.

Simbas, ambayo ina kocha mpya Ian Snook kutoka New Zealand, itaanza kampeni yake dhidi ya Morocco jijini Casablanca mnamo Juni 23.

Itakabana koo na Zimbabwe, Uganda na Tunisia mnamo Juni 30, Julai 7 na Agosti 11 jijini Nairobi kabla ya kukamilisha kampeni yake dhidi ya mabingwa watetezi Namibia jijini Windhoek hapo Agosti 18.