Habari

Simhitaji Uhuru kupenya Mlima Kenya, adai Raila

February 28th, 2020 2 min read

Na PETER MBURU

KIONGOZI wa chama cha ODM Raila Odinga amesema kuwa hahitaji kushikwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta ili kupenya Mlima Kenya, akisema tayari ana uhusiano ulioanza zamani na eneo hilo na kuwa anakubalika kivyake.

Bw Odinga amejitaja kuwa shemeji na rafiki wa Mlima Kenya na kuwa wakazi wa eneo hilo wanampenda kutokana na uhusiano wake na viongozi wa mbeleni eneo hilo, na kuwa uhusiano wake na Mlimani ulianza enzi za babake Oginga Odinga.

Alipoulizwa ikiwa anaogopa kwenda eneo hilo ama anahitaji kwenda na Rais Kenyatta katika runinga ya Ktn News Jumatano, Bw Odinga alisema haogopi chochote.

“Mimi siogopi kwenda Mlima Kenya kwa kuwa fulani amesema (kitu), hayo yote ni maneno ya uzushi. Nakwenda kama rafiki ya Wakikuyu, naenda kama muthoniwa (shemeji), naenda kwa athoni (mashemeji),” Bw Odinga akasema.

Alieleza jinsi babake, Oginga alikataa wadhifa wa Waziri Mkuu ili Rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta aachiliwe; jinsi alifungwa pamoja na wanasiasa wa eneo hilo Kenneth Matiba na Charles Rubia miaka ya tisini; na alivyompigania Rais Mstaafu Mwai Kibaki hadi akashinda, akisema mifano hiyo yote ni msingi tosha wa kumpenyeza eneo hilo.

“Wakazi wa eneo hilo wananipenda. Hata Kibaki alipopata ajali wakati wa kampeni, nilitangaza kuwa japo nahodha (Kibaki) amejeruhiwa, sharti mchezo ungeendelea na nikasimamia kampeni. Tulipompeleka Kibaki Othaya, njiani nilikuwa nikiitwa Mutongoria Njamba (kiongozi shujaa) na Wakikuyu,” akasema.

Alitaja pingamizi za viongozi wafuasi wa Naibu Rais William Ruto eneo hilo dhidi yake (Raila) kuwa kelele za chura, na ambazo hazingemzuia kwenda Mlima Kenya.

“Waswahili husema migurumo za chura haizuii ng’ombe kunywa maji, yale unaskia ni ngurumo za chura, ngombe atakunywa maji,” akasema, akijirejelea kuwa ng’ombe na chura kuwa wafuasi wa Dkt Ruto Mlimani.

Kiongozi huyo Jumanne alikutana na viongozi wa eneo hilo, wakihusisha magavana Kiraitu Murungi (Meru), Anne Waiguru (Kirinyaga), Muthomi Njuki (Tharaka Nithi) na wabunge Kanini Kega (Kieni) na Maina Kamanda, kujadili kuhusu mkutano wa Mpango wa Maridhiano (BBI) uliopangwa kuandaliwa Meru kesho.

Bw Odinga alisema tayari viongozi wa eneo hilo wamemkaribisha, ishara kuwa eneo hilo halina ubaya naye.

“Tuliongea juu ya mambo ya maendeleo eneo hilo, kilimo, elimu, usalama na kadhalika na wakanikaribisha wenyewe kutembea huko,” akasema.

Matamshi yake yamekuja wakati kumekuwa na gumzo kuwa anajaribu kumtumia Rais Kenyatta na BBI ili akubalike Mlimani, na kuwa kuna pingamizi kali dhidi yake.

Lakini alishikilia kuwa maneno hayo si ya kweli, akisema yeye ni shemeji wa Mlimani, na “damu ni nzito kuliko maji.”