Simiyu atumai Oluoch, Keyoga watapona kabla ya Edmonton 7s kusaidia Shujaa

Simiyu atumai Oluoch, Keyoga watapona kabla ya Edmonton 7s kusaidia Shujaa

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Innocent ‘Namcos’ Simiyu anatumai kuwa wachezaji Jeffrey Oluoch na Derrick Keyoga watakuwa sawa kwa duru ya pili ya Raga za Dunia 2021 itakayofanyika jijini Edmonton, Canada mnamo Septemba 25-26.

Oluoch kutoka klabu ya Homeboyz na Keyoga anayechezea Menengai Oilers walipata majeraha katika duru ya kwanza iliyoandaliwa jijini Vancouver mnamo Septemba 18-19.

“Oluoch aliumia kifundo cha mkono naye Keyoga alipata jeraha la kifundo cha mguu. Natumai watakuwa sawa wakati wa Edmonton Sevens ili watusaidie katika juhudi zetu za kutafuta mafanikio zaidi,” Simiyu aliambia Taifa Leo hapo Septemba 22.

Aidha, Simiyu alisifu wachezaji Alvin Otieno, Daniel Taabu na Oluoch kwa kuwa miongoni mwa wachezaji waliong’ara kiasi cha kutambuliwa na Shirikisho la Raga Duniani kwa mchango wao kwa Shujaa jijini Vancouver ambako timu hiyo ilifika fainali. Shujaa ilichapwa 38-5 na Afrika Kusini katika fainali hiyo yake ya kwanza tangu Aprili 2018.

“Tunafurahi sana kuwa kazi ya kila mmoja wao na tunatumai watafanya bora zaidi,” alisema.

Simiyu alifichua kuwa Shujaa ilipimwa virusi vya corona mnamo Septemba 17, 20 na 22 na hakuna kisa chochote kilipatikana.

Mabingwa hao wa duru ya Singapore Sevens mwaka 2016 walifanya mazoezi yao ya kwanza tangu duru ya Vancouver mnamo Septemba 21 na pia Septemba 23.

Timu hiyo italimana na Chile, Uhispania na Amerika katika mechi za Kundi B jijini Edmonton.

Kundi A linajumuisha Canada, Hong Kong, Afrika Kusini na Mexico. Ireland, Jamaica, Uingereza na Ujerumani zinapatikana katika Kundi C.

Mataifa 12 yanashiriki Raga za Dunia mwaka huu. Argentina, Australia, Fiji, France, Japan, New Zealand na Samoa hazikusafiri Canada kutokana na changamoto za janga la virusi ya corona.

You can share this post!

Rising Starlets wajitia makali kwa mchuano wa kuingia Kombe...

TAHARIRI: Sarakasi hazimfai raia anayeumizwa