Simiyu afurahishwa na matayarisho ya Shujaa

Simiyu afurahishwa na matayarisho ya Shujaa

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Innocent ‘Namcos’ Simiyu amefurahishwa na jinsi maandalizi ya timu ya taifa ya Kenya Shujaa yanavyoendelea kwa duru mbili zijazo za Raga za Dunia zitakazofanyika Uhispania.

Shujaa iliingia kambi ya kutotangamana na watu kutoka nje ugani Kasarani mnamo Januari 3 kwa hofu ya maambukizi ya virusi vya corona na pia kumakinikia bora zaidi matayarisho yake.

Itakabiliana na Canada na Wales katika mechi mbili za kwanza za Kundi D za Malaga Sevens mnamo Januari 21 kabla ya kukamilisha awamu ya makundi dhidi ya Ufaransa mnamo Januari 22. Duru hii ina mataifa 17 baada ya Ujerumani kualikwa.

“Nina wachezaji 27 kambini, lakini tutapunguza kikosi cha msimu huu hadi 24 mwisho wa Januari. Maandalizi yamekuwa mazuri. Tunamakinikia zaidi uanzishaji wa mpira na umilikaji. Nitataja kikosi cha Malaga Sevens hapo Jumatano,” Simiyu aliambia Taifa Leo baada ya mazoezi ya Jumatatu asubuhi.

Malaga Sevens itafuatiwa na Seville Sevens mnamo Januari 28-30. Shujaa inakamata nafasi ya nane kwa alama 22 baada ya duru mbili za kwanza zilizofanyika Dubai mwezi Novemba na Desemba 2021.

You can share this post!

Morocco wakomoa Ghana katika gozi kali la Kundi C kwenye...

Mudavadi ayumba uchaguzi ukibisha

T L