Simu 2 zilizotupwa na magaidi waliotoroka Kamiti zapatwa Kitui

Simu 2 zilizotupwa na magaidi waliotoroka Kamiti zapatwa Kitui

Na KITAVI MUTUA

SIMU MBILI za mkononi na diski zilizopatikana katika eneo walikokamatiwa magaidi watatu hatari waliotoroka gereza la Kamiti na kusafiri zaidi ya kilomita 300 bila kugunduliwa, huenda zikafichua walivyopanga njama ya kuhepa.

Vifaa hivyo vilipatikana Kamuluyuni, Kaunti ya Kitui na inaaminika kuwa ni magaidi hao waliovitupa muda mfupi kabla yao kukamatwa na polisi wa akiba.Pia, siku tatu baada ya kukamatwa, karatasi nyeupe iliyokuwa imeandikwa nambari tatu za simu ilipatikana imetupwa kwenye kichaka.

Kulingana na mkuu wa polisi wa akiba eneo hilo, Bw Komu Kilonzi, walipata simu ambazo magaidi hao walitumia kuwasiliana na wenzao katika msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu zikiwa zimevunjwa na kuharibiwa.

“Tumekuwa tukitafuta vichakani kwa kuwa tulipowakamata Alhamisi, magaidi hao walikiri kwamba walikuwa na simu za mkono ambazo walipoteza wakiwa kichakani wakifukuzwa,” alisema Bw Kilonzi.

Alisema walipata diski ambayo yaliyomo hayakubainika mara moja huku simu hizo zikipatikana maeneo tofauti karibu na walipokamatiwa. Inaonekana walivunja simu hizo kuziharibu ili kuharibu habari na ushahidi wowote ambao zingetoa kwa wachunguzi kuhusu kutoroka kwao kulivyopangwa na watu waliowasiliana nao.

Uchunguzi wa mwanzo unaonyesha kuwa magaidi hao Musharaf Abdalla Akhulunga, maarufu kama Zarkawi, au Alex, au Shukri, Mohamed Ali Abikar na Joseph Juma Odhiambo anayefahamika pia kama Yusuf, walikuwa wakitegemea ramani za mtandao wa Google kutafuta njia. na walikuwa wakiwasiliana na wenzao katika msitu wa Boni.

Simu hizo mbili, diski na karatasi iliyoandikwa nambari za simu zilikabidhiwa wachunguzi wanaotoka kitengo cha polisi wa kukabiliana na ugaidi na Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI).Kamanda wa polisi kaunti ya Kitui Leah Kithei alisema kwambza kupatikana kwa vifaa hivyo kutafichua kitendawili cha kutoroka kwa magaidi hao.

You can share this post!

Gor kupiga mechi tatu kujiandalia Caf

Kaunti kuadhibu ‘makanjo’ dhalimu

T L