Habari Mseto

Simulizi ya mvulana mkimbizi aliyezoa alama 410 na kujiunga na shule ya kitaifa

January 29th, 2024 1 min read

NA RICHARD MAOSI

FAMILIA ya Anjelo Odura ilitoroka taifa la Sudan Kusini kwa sababu ya mapigano ya mara kwa mara baina ya koo na mbari.

Walipata makao mapya katika Kambi ya Wakimbizi ya Kakuma, Kaunti ya Turkana wakitarajia kwamba hali itakuwa shwari warejee nyumbani.

Baada ya kusubiri kwa muda mrefu tangu 2016, Anjelo aliridhia hali akaamua kujikaza kisabuni ili aje kufaulu maishani.

Kwenye mahojiano maalum na Taifa Leo Dijitali, kijana Anjelo alidokeza kwamba alizoa jumla ya alama 410 katika Mtihani wa Kitaifa Darasa la Nane (KCPE) 2023.

Akiwa mtoto wa nne katika familia ya watoto saba, mvulana huyu anasema mara nyingi alikuwa akimsaidia mama yake kulea ndugu zake wachanga.

Wakati kidogo uliobakia alitumia kusoma.

Katika Kambi ya Kakuma familia yake ilikuwa ikitegemea misaada kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa ambalo hutumika kulinda maslahi ya wakimbizi (UNHCR).

Mwaka 2023, mwalimu aliyekuwa akimfunza kambini alimsaidia kupata ufadhili kujiunga na Shule ya Msingi ya AC Kamusinga, Kaunti ya Bungoma.

Hapa alichukua mwaka mmoja tu na kushangaza wengi alipozoa alama 410 na kuibuka wa kwanza.

Matokeo yalipotangazwa walimu wake walimsaidia kuchangisha hela kutoka Kakuma hadi Kaunti ya Kericho ambako alikuwa ameitwa kujinga na Shule ya Kitaifa ya Kabianga.

Walimu walifanikiwa kuchanga Sh3, 500 ingawa alikuwa akihitaji Sh4, 000 kufika Kericho.

Kabla ya kuondoka Kakuma alitumia kila mbinu kumshawishi makanga wa gari ambalo lilimsafirisha hadi Kericho, hii ikiwa ni mara yake ya kwanza kuzuru Kaunti nyingine nje ya Turkana.

Bila karo wala bidhaa za kutumia alipokelewa na usimamizi wa shule na kuanza rasmi masomo yake.

Bw Ezekiel Kurgat ambaye ni mwalimu mkuu wa Shule ya Kabianga, anasema ilibidi ampokee Anjelo kwa sababu hii sio mara ya kwanza kushuhudia visa kama hivyo.

“Ataendelea kupata mafunzo hapa hadi apate mfadhili wa kugharamia masomo yake yote,” akasema.