Habari

'Sina deni la Ruto 2022'

February 1st, 2020 2 min read

WAIKWA MAINA Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta alipasua mbarika Ijumaa na kutangaza kuwa hana deni lolote la kisiasa la naibu wake, Dkt William Ruto kuhusu uchaguzi mkuu wa 2022.

Rais alisisitiza kuwa hataunga mgombeaji yeyote wa urais kwenye uchaguzi huo na akawataka wanaomezea mate kiti hicho akiondoka mamlakani wajipange kivyao.

Tamko lake linanuiwa kutia kikomo shinikizo za wandani wa Dkt Ruto ambao wamekuwa wakimtaka amrudishie mkono kwa kumuunga tangu uchaguzi mkuu wa 2013.

Akiongea katika kituo cha kibiashara cha Githioro, eneobunge la Kinangop katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo, Rais Kenyatta alisema Wakenya ni werevu na hawahitaji kuelekezwa kuhusu wanayefaa kuchagua kuwa kiongozi wao.

“Wakenya ni watu werevu na watafanya uamuzi wa busara 2022. Hawahitaji mwongozo kutoka kwangu au mtu mwingine yule,” alisema Rais Kenyatta.

Wandani wa Dkt Ruto, maarufu kama Tangatanga, wamekuwa wakizunguka nchini kumpigia debe wakiambia Wakenya kwamba ndiye anayefaa kumrithi Rais Kenyatta.

Ijumaa, Rais alisema kwamba Wakenya wanawatazama na kuwasikiliza viongozi wote kwa makini na ni vitendo vyao vitakavyowafanya wapigakura kuamua atakayewaongoza kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Katika hatua inayoonyesha kwamba, hana mipango ya kushirikiana tena na Dkt Ruto na wabunge wanaomuunga mkono, Rais Kenyatta alisema wamekuwa wakimdanganya kuwa wanaanzisha miradi ya maendeleo ya kusaidia Wakenya na hatawaamini kamwe.

“Sitaamini yeyote, kuna wale niliokuwa nikituma kuniwakilisha na kuhakikisha miradi ya maendeleo imetekelezwa lakini wakaanza kuwa na tabia ya fisi na kufanya mambo yao ya kujipatia utajiri, msidanganywe na yeyote kwamba nimemtuma, kuanzia leo (Ijumaa) sitatuma yeyote kunisaidia, nitakuwa nikijiwakilisha mwenyewe,” alisema.

Dkt Ruto amekuwa akitembelea maeneo tofauti akiandamana na wandani wake akisema huwa ametumwa na Rais kukagua miradi ya maendeleo.

Hata hivyo, Rais Kenyatta alisema watu aliotuma kumsaidia kutimiza ajenda ya maendeleo ya serikali yake wamemsaliti na kuanza kumtusi wakipinga handisheki yake na kiongozi wa ODM Raila Odinga na mchakato wa maridhiano( BBI).

“Nimekuwa nikikumbusha viongozi kwamba tulichaguliwa kuhudumia Wakenya na sio kuendeleza siasa lakini hawasikii. Nimeshangaa kupata maeneo mengi ya Kinangop hayana stima ilhali kiongozi wenu amekuwa akizunguka kaunti nzima akijadili siasa na kunitusi. Hawa watu wamekuwa wakija kwangu kunidaganya wanafanyakazi na kila kitu kiko sawa mashinani,” alisema Rais Kenyatta.

Alimwambia Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti hiyo Faith Wairimu Gitau na mbunge wa Kinangop Zachary Thuku ambao ni wandani wa Dkt Ruto kwamba, lengo lake ni kuhakikisha watoto wote wamejiunga na shule na bei za mazao ya kilimo zimeimarika na sio kuendeleza siasa.

“Wale wote wanaozunguka nchi wakieneza chuki na kunitusi wamefanya nini kutatua shida zinazowakabili. Ni watu waliojawa na ubinafsi na kujali matumbo yao. Wacha waendelee kutukana tunaposonga mbele,” alisema na kumsifu Gavana wa Kaunti ya Nyandarua kwa kumweleza ukweli kuhusu mateso wanayopitia wakazi wa kaunti yake huku wengine wakimdanganya.

Rais Kenyatta alisema hataki kutumia BBI kujinufaisha bali anataka kuepusha Wakenya kumwaga damu kila wakati baada ya uchaguzi.

“Ni mama zetu, dada na ndugu zetu wanaoteseka wakati wa ghasia za kisiasa, nitakuwa mahali salama kama viongozi wengine mkipigana baada ya uchaguzi na haya ndiyo sitaki yatendeke, yangu ni kuhakikisha uchaguzi wa amani, wacheni wanaotaka kuchaguliwa wapigane vita vyao,” kiongozi wa nchi alisema.

Lakini Bw Kimemia alisisitiza kuwa Rais Kenyatta ana umri mdogo kustaafu siasa akikamilisha kipindi chake cha pili 2022 na anapaswa kuwa katika serikali ijayo.