Habari MsetoMakalaSiasa

Sina haja na urais 2022 – Uhuru

June 20th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amepuuzilia mbali madai kuwa anapania kutumia mabadiliko ya Katiba kuendelea kusalia mamlakani baada ya 2022.

Aidha, alikanusha uvumi unaosambazwa na mahasidi wake wa kisiasa kwamba anakimezea mate kiti cha Waziri Mkuu mwenye mamlaka, kinatakachobuniwa baada ya mageuzi hayo ya katiba kupitia kura ya maamuzi.

“Inasikitisha kuwa kuna watu wanaofasiri mageuzi ya Katiba kupitia kura ya maamuzi kuashiria kuwa ni njama ya kuongeza muhula wangu uongozini kama rais. Na wengine pia wamedai eti ninataka kuwa Waziri Mkuu. Madai haya hayana ukweli wowote,” Rais Kenyatta akasema Alhamisi jioni.

Alikuwa akijibu maswali, kwa njia ya video, wakati wa mkutano na shirika la Atlantic Council lenye makao yake nchini Amerika.

Rais akaongeza: “Nawaambia, ikiwa kuna suala ambalo Wakenya wanafahamu fika ni mihula miwili ya urais. Wakenya wamefahamu kuwa marais wamekuwa wakihudumu kwa mihula miwili tangu 1992 utawala wa vyama vingi uliporejelewa nchini Kenya. Hakuna Rais ambaye amewahi kuvunja sheria hiyo na sina nia ya kuwa wa kwanza kufanya hivyo.”

Kiongozi wa taifa alisema lengo la Mpango wa Maridhiano (BBI), na mageuzi yanayopendekezwa kwayo, ni kuhakikisha kuwa vizazi vijavyo havikabiliwa na baadhi ya changamoto zinazokumba kizazi cha sasa.

“Chini ya utawala wa vyama vingi, taifa hili limekuwa likishuhudia machafuko kila baada ya chaguzi. Kwa hivyo, ushirikiano wangu na Raila (Odinga) unalenga kujaribu kuona kama tutapata suluhu la matatizo kama hayo kupitia mpango wa BBI,” Rais Kenyatta akaeleza.

Kuhusu iwapo maguezi ya Katiba yanalenga kubuni cheo cha Waziri Mkuu alisema: “Sina habari kama kama kutabuniwa wadhifa wa waziri mkuu katika katiba. Haya ni maoni ya baadhi ya watu. Kile ambacho raia wana haja nayo ni kupata thamani ya kura yao, ugavi sawa wa rasilimali na uwepo wa serikali inayowashirisha watu wote.”

Naibu Rais William Ruto, na wanasiasa wandani wake, wamepinga pendekezo la mageuzi ya katiba kupitia kura ya maamuzi ili kubuniwe wadhifa wa Waziri Mkuu na manaibu wake wawili, wakisema zitawaongezea raia gharama zaidi.

Baadhi yao wamekuwa kuwa aidha, Rais Kenyatta anapania kusalia mamlakani baada ya muhula wake wa pili na wa mwisho kukamilika au anataka ateuliwa Waziri Mkuu baada ya 2022.

Lakini kwenye mahojiano hayo, yaliyoendeshwa na Katrina Manson, Rais Kenyata alisema hangezungumzia suala hilo la Waziri Mkuu “kwa sababu sio suala kuu katika mpango mzima wa BBI”.

“Kile ninaweza kusema ni kuwa Afisi iliyoko sasa ni ile ya Rais. Rais wa Jamhuri ya Kenya. Na Katiba yetu imebainisha wazi kuwa Rais huhudumu kwa mihula miwili. Mihula miwili pekee. Na sasa niko katika muhula wangu wa pili,” akasisitiza.