Habari MsetoSiasa

Sina muda wa kumtembelea Ruto Karen – Moi

May 9th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

SENETA wa Baringo Gideon Moi amepinga madai kwenye mitandao ya kijamii kuwa alikutana na Naibu Rais William Ruto nyumbani kwake mtaa wa Karen, Nairobi, akiyataja kuwa propaganda.

Bw Moi alitaja madai hayo kuwa uvumi usio wa kweli ambao unaendeshwa na wanasiasa wa mrengo fulani, ili kuwahadaa Wakenya.

Seneta huyo, ambaye ni hasimu mkubwa wa Dkt Ruto alisema amekuwa Kabarak na Rais Mstaafu Daniel Moi “ninapotumia muda inavyofaa.”

“Mitandao ya kijamii imekuwa ikiwaka kwa picha zinazodai kuwa nilikuwa katika boma fulani Karen. Habari hizo si za kweli, wala ni propaganda kutoka kwa mrengo fulani wa kisasa unaotaka kuwahadaa Wakenya. Nimekuwa nyumbani Kabarak tangu jana ambapo tunatumia muda vizuri na Mzee,” akasema Bw Moi.

Tanguu Alhamisi saa za asubuhi, picha zilikuwa zikizungushwa mitandaoni kudai kuwa seneta huyo walikuwa wamekutana na kuzungumza na Naibu Rais, madai ambayo yalikuwa yamechangamsha Wakenya, hasa kwa vile wawili hao wamekuwa na tofauti kubwa.

Lakini mwenyekiti huyo wa chama cha KANU aliweka mambo wazi kuwa bado hayuko tayari kwa hilo, kukosa kumtaja Dkt Ruto, wala kutaja nyumbani kwake kukionyesha kiwango cha uhasama baina yao.