Habari MsetoSiasa

Sina muda wa kuvuruga Jubilee, nina kazi nyingi AU – Raila

March 10th, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

KIONGOZI wa chama cha ODM Raila Odinga, Jumamosi alipinga madai kuwa anaingilia chama cha Jubilee na shughuli za serikali na hivyo kusababisha migogoro.

Bw Odinga aliwaambia wanaodai hivyo kuwa sasa yeye hashughuliki na masuala madogo ya humu nchini, ila yale yanayoathiri bara zima la Afrika.

Aliwataka wanaomhusisha na mizozo katika chama hicho kuacha kupoteza muda kwani yuko katika ngazi tofauti. Aliongeza kuwa ushirikiano wake na Rais Uhuru Kenyatta ni kwa manufaa ya taifa wala si kujitafutia umaarufu kabla ya uchaguzi wa 2022.

“Raila hajawahi kuwa katika Jubilee, yeye ni mwanachama wa ODM, huwa hahudhurii mikutano ya Jubilee ili aambiwe kuwa analeta utengano katika chama hicho na pia hahudhurii mikutano ya mawaziri ili aambiwe kuwa anazua mgawanyiko huko,” akasema.

Kiongozi huyo alieleza hayo alipokuwa akihutubu katika hafla ya kuadhimisha mwaka tangu walipoafikiana na Rais Kenyatta, katika hoteli ya Serena, Jijini Nairobi.

Alisema yeye sasa anashughulika na majukumu aliyopewa katika Muungano wa Afrika (AU) , na hivyo masuala ya kitaifa ni madogo sana kwake.

“Ikiwa ninaingilia chochote, basi ninaingilia katika muungano wa AU ambapo nina majukumu, sio hapa, sasa mimi nacheza ‘Super League’, hii ligi ya nyumbani nimewaachia. Mimi sasa nacheza huko juu na Ronaldo na Messi,” akasema kiongozi huyo.

Bw Odinga alisema haya baada ya kueleza kuwa muafaka baina yake na Rais Kenyatta haukuwa na nia ya kumlenga yeyote, na kutetea vita vinavyoendeshwa dhidi ya ufisadi kuwa havimlengi mtu ama jamii yoyote.

“Sisi wawili hatutaki kupata chochote kutokana na hili, sote tunataka kuacha nchi ikiwa na sifa nzuri. Hatumlengi yeyote, juhudi hizi ni za kuunganisha watu wote.Vita dhidi ya ufisadi havilengi mtu ama jamii yoyote. Ufisadi ni saratani ambayo sharti tukabiliane nayo nchini,” akasema Waziri Mkuu wa zamani.

Kiongozi huyo aidha alieleza kuwa kamati waliyounda na Rais inaendelea kukusanya maoni kutoka kwa Wakenya, na kusisitiza kuwa marekebisho ya katiba yataandaliwa.

Bw Odinga alidokeza kuwa nafasi kadha za uongozi zitaongezwa serikalini, siku mbili tu baada ya Naibu Rais William Ruto kukosoa hatua ya kutaka nafasi zaidi za uongozi kuongezwa, kupitia kura ya maoni.

“Tumevaa viatu hivi (katiba) kwa miaka tisa sasa, na tunajua ambapo vinatuathiri, sasa tunaweza kurekebisha mahali palipo na shida na kuongeza kitu palipo na upungufu,” akasema Bw Odinga.

Akifunga kongamano la ugatuzi mnamo Alhamisi, Naibu Rais alikashifu wanaopanga kufanyia katiba marekebisho ili kuongeza nafasi za uongozi kuwa wamepotoka, akitaja wazo hilo kuwa lisilo la busara.

“Asilimia 52 ya mapato ya nchi huishia katika mishahara ya wafanyakazi, chini ya asilimia 20 pekee zikisalia kwa miradi ya maendeleo. Kwa kuzingatia haya, kupendekeza kuwa nyadhifa zingine za uongozi ziongezwe ni kukosa kufikiria, isiyokuwa na msingi wowote na yenye kukosa mwelekeo,” Dkt Ruto alisema.