Michezo

Sina nia ya kustaafu soka hivi karibuni – Zlatan Ibrahimovic

December 12th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

NYOTA Zlatan Ibrahimovic, 39, amesema hayuko tayari kuondoka kwenye ulingo wa soka hivi karibuni kwa kuwa angali na kiu ya kujipa mafanikio zaidi katika mchezo huo.

Fowadi huyo wa AC Milan kwa sasa ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) msimu huu baada ya kufunga mabao 10 kutokana na mechi nane za ufunguzi. Mabao hayo yanamweka mbele ya Cristiano Ronaldo wa Juventus na Romelu Lukaku wa Inter Milan.

Ibrahimovic ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Uswidi anajivunia rekodi ya kuchezea Ligi Kuu za mataifa saba tofauti katika kipindi cha zaidi ya miaka 20 ya kitaaluma.

“Nitazidi kujituma uwanjani hadi nitakaposhindwa kabisa kufanya baadhi ya vitu ninavyofanya kwa sasa. Muhimu zaidi nidumishe hali nzuri ya mwili na mengine yatazidi kujidhihirisha,” akasema.

Kufikia sasa, AC Milan ambao hawajapoteza mechi yoyote kati ya 10 zilizopita, wanaongoza msimamo wa jedwali la Serie A kwa alama 26, tano zaidi kuliko nambari tatu Inter Milan.

“Kikosi kinajivunia fomu ya kutisha na tunazidi kufanya vyema msimu huu. Timu inatawaliwa na kiu ya kusajili ushindi katika kila mchuano na lengo letu ni kutwaa ubingwa wa taji la Serie A,” akaongeza Ibrahimovic ambaye alikosa mechi mbili za waajiri wake baada ya kuugua Covid-19 mwanzoni mwa msimu huu wa 2020-21.

Ibrahimovic ambaye pia amewahi kuchezea kikosi cha LA Galaxy nchini Amerika, anajivunia kufunga zaidi ya mabao 500 katika soka ya kitaaluma. Amewahi pia kuvalia jezi za Manchester United, Barcelona, Inter, Ajax, Paris St-Germain na Malmo.